728x90 AdSpace

  • Latest News

    Sunday, October 04, 2015

    UCHAMBUZI YAKINIFU MECHI KUBWA SITA WIKENDI HII,EPL,BUNDESLIGA,LIGUE 1,LA-LIGA NA EREDIVISIE..........

    KWA TAARIFA YAKO:

                 NA
              
                    MR'CHOI


    Kwa mara nyingine tena tunakutana katika anga hili la soka lenye kila radha na kachumbari yenye mchanganyiko wa kipekee.

    Najua gumzo kubwa katika medali ya soka la kibongo ni sakata la Nyosso ambapo naona kuna wachambuzi wanajitaftia ushujaa wa kijinga kupitia hili swala ila pia kumbuka jambo jingine ambalo limeteka hisia za wadau wa soka ni rekodi ya C.Ronaldo kufikisha magoli 500 katika historia ya kucheza kwake soka huku akifanikiwa kuwa mfungaji wa muda wote wa Real Madrid.

    Pasipo kuchelewa ngoja siku ya leo tujikite Barani Ulaya sehemu ambayo ni kiburudisho tosha cha mchezo wa soka.

    Skia juma hili kuna mechi nyingi sana ambazo zimeteka kila kona yenye wanamichezo kule Ufaransa kuna mchezo wa Psg dhidi ya Marseille kule Uholanzi kuna utamu wa Psv dhidi ya Ajax nikichungulia pale Ujerumani kuna ngoma ya kusisimua kati ya Bayern Munich dhidi ya Dortmund.

    Wakati nikigeuka kushoto pale Hispania ni Real Madrid dhidi Athletico Madrid nikitupa jicho la upande wa Kulia pale Visiwa vya Malkia Uingereza kuna kimbembe cha Arsenal watakao pambana na Manchester United huku pale katika Jiji la Liverpool ni kimuhemuhe cha ndugu wawili Liverpool na Everton.

       :::::                            PSG VS MARSEILLE

    Le Classique

    Nikianza kuangaza mchezo wa Psg na Marseille ni mchezo mkubwa kwa ukubwa wa majina ya timu hizi lakini nikiangaza uhalisia wa sasa hivi Marseille hana cha kupata mbele ya kikosi cha Blanc.

    Kwa mara ya kwanza timu hizi zilikutana tarehe 12/12/1971 mara ya mwisho ni msimu uliomalizika wa 2014/2015 na kushuhudia Psg wakiibuka na ushindi wa goli 3-2 na kwenye historia ya vilabu hivi pindi vikikutana ushindi mkubwa zaidi ni ule wa 8/1/1978 kwa Paris Saint German kuibuka na ushindi wa goli 5-1.

    Siku zinavyo zidi kwenda ndivyo ambavyo tunashuhudia kiwango kibovu cha Marseille msimu huu tofauti na wapinzani wao Psg timu ambayo imekamilika kila Idara huku Marseille wakiteswa na ubutu wa safu ya ushambuliaji lakini pia safu ya ulinzi haipo vyema hivyo wanakazi ya kufanya walau wapate pointi moja mbele ya Psg ambayo ipo katika hali ya ushindi na uimara wa sehemu zote tatu safu ya Ulinzi,Kiungo na Safu ya Ushambuliaji.

    Ukiangaza katika msimamo Psg ni vinara wakiwa na pointi  20 wakati Marseille iliyo chini ya kocha raia wa Hispania Jose Miguel aliechukua nafasi ya Muargentina Marcelo Bielsa anawakati mgumu kwani wana pointi 8 wakiwa nafasi ya 15

    Kuwashinda Psg panahitaji kazi ya ziada kwa maana hiyo bado kwa kiwango cha Marseille hivi sasa Psg wananafsi kubwa ya kushinda mchezo huu ambao hutawaliwa na ubabe mwingi na kwa mchezaji kupewa kadi nyekundu si jambo la kushtusha.

    ::::::::                                              AJAX VS PSV

    Nikiangaza kule kwa jamaa zangu Uholanzi tutashuhudia wafalme wawili wa soka Nchini humo Psv dhidi ya Ajax timu ambazo zimekuwa na utawala wa kupokezana katika Ligi yao.

    Kumbuka Ajax wametwaa ubingwa wa Eredivisie mara 25 huku utawala wao wa mwisho ni msimu wa 2013-2014 lakini wapinzani wao Psv wakitwaa ndoo mara 19 ambapo kwa sasa ni mabingwa watetezi.

    Ukiangaza takwimu za vilabu hivi pindi zikikutana kumekuwa na ushindani mzuri kwani hata katika upande wa takwimu hawaja achana sana wamekutana mara 129 mara ya kwanza ikiwa ni 12/4/1931 Ajax akiibuka na ushindi wa goli 4-2 na kwa ujumla Ajax kashinda mara 56 huku Psv akishinda michezo 51.

    Kwa muangazo wa ushindani wa sasa ni vigumu kubashiri  ushindi mkubwa kwa timu moja wapo kama ule wa tarehe 22/11/1964 Ajax alipo shinda 5-0.

    Kocha wa sasa wa Ajax beki wao wa zamani Franciscus de Boer msimu huu timu yake imekuwa na matokeo mazuri wakiwa hawaja poteza mchezo hata mmoja wakitoa sare moja na kuwa kileleni kwa pointi 19 wakati mpinzani wake kiungo wa zamani wa Psv kocha wa sasa Phillip Cocu bado hawajawa na msimu mzuri wakiwa na pointi 14.

    Ajax wako vyema katika safu ya ulinzi huku jicho lao likiwa ni mshambuliaji El Ghazi huku Psv walio wazuri kushambulia kupitia pembeni wakimtegemea De Jong.

    Kwa tasmini ya uhalisia Ajax ana nafasi kubwa kushinda mbele ya Psv kutokana ma uimara wao hasahasa safu ya Ulinzi.

    :::::::::                      BAYERN MUNICH VS DORTMUND

    Der Klaassiker

    Sasa Tuangaze kule Ujerumani ambapo kuna ngoma tamu na yenye radha ya kipekee Bayern Munich na Dortmund.

    Unajua soka la Ujerumani lina radha ya kipekee sana kutokana na ushindani wa vilabu vyao licha ya ligi kuonekana ya mtawala mmoja ambae ni Bayern Munich.

    Unajua katika mchezo huu hakuna haja ya kuangalia historia kutokana na ubora wa vikosi vya timu zote msimu huu.

    Tunaona kikosi cha Guardiola bado kimezidi kupata ushindi wa asilimia 100 huku kikosi kikichagizwa na kiungo Douglas Costa ambae amekuwa na kiwango bora kabisa katika msimu wake wa kwanza ndani ya Bavarian.

    Ubora wa Bayern msimu huu umetufanya tuzidi kuona ubora wa mshambuliaji raia wa Poland Robert Lewandowski ambae ndani ya michezo mitatu ya karibuni kafunga magoli 10.

    Dortmund ujio wa kocha mpya Thomas Tuchel msimu huu umefanya tuione Dortmund mpya ambayo mpaka sasa
    katika michezo 14 michuano mbalimbali  hawaja poteza wameshinda michezo 11 na kutoa sare 3 huku timu ikionekana kuwa nzuri zaidi katika safu ya ushambuliaji ambayo Muafrika Pierre Aubameyang akiwa katika kiwango bora kabisa kwani mpaka sasa katika ligi anagoli 9 nyuma ya Lewandowski mwenye magoli 10.

    Sasa ukija katika uhalisia utagundua Bayern ni timu ambayo imesukwa na kuimalika sehemu zote tofauti na Dortmund ambayo bado safu ya ulinzi inaruhusu magoli kizembe licha ya uhodari wa safu ya ushambuliaji.

    Ni mchezo ambao utakuwa na presha kubwa kwa uhalisia wa ushindani katika ligi Bayern ni vinara wakiwa na point 21 huku Dortmund wakiwa na point 17 kwa maana hiyo Dortmund wanahitaji punguza gepu la pointi na ili wawe na ndoto za ubingwa basi walau washinde mchezo huu.

    Kwa uimara wa vikosi vyote wala usitaraji kuiona historia ya 27/11/1971 pale ambapo Bayern alishinda goli 11-1 Dortmund na safari hii kuna kimbembe kizito kwani timu hizi zimekutana mara 108 huku Bavarian wakishinda mara 49 kwa maana hiyo wanautafuta ushindi wa 50 wakati Die Borussen wameshinda michezo 29 wakitafuta ushindi wa 30 au pengine tukashuhudia sare ya 31.

    Kwa kutumia kaunta na kupita pembeni kwa maana ya krosi itakuwa chagizo la ushindi kwa Dortmund lakini wanatakiwa kuwa makini sana upande wa Costa ambao ni hatari zaidi.

    Tusubiri tuone kama Bayern wataandika historia ya Bundesliga kwa kushinda michezo 8.

    ::::                 ATHLETIC MADRID VS REAL MADRID

      El-Derbi Madrileno

    Hilo ndo jina linalo tamkwa zaidi nchini Hispania hususani viunga vya Jiji la kifalme Madrid.

    Wajanja wa mitaa hiyo wanafananisha vita vya watoto wa Uswazi dhidi ya watoto wa kishua.

    Unajua radha ya Charanga sharti uicheze ingawa lazima uwe mwepesi  wababe hawa wamekutana mara 210 huku Real Madrid wakiibuka na ushindi mara 107 sare 50 na Atletico Madrid wakishinda michezo 53.

    Katika La-Liga Real Madrid wameshinda mara 85 wapinzani wao wakishinda mara 38 sare 33  katika michezo 156.

    Msimu uliopita tulishuhudia dhahma kwa Real kupigwa michezo yote ya ligi nyumbani na ugenini kwa kufungwa 2-1 na 4-0.

    Rojiblancos ambao ni Atletico Madrid imekuwa ni timu inayo cheza kitimu zaidi licha ya kutokuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa kama Real Madrid.
      
      Simeone kaijenga timu yake kwa misingi ya kupambana kwapamoja pasipo kutegemea kiwango cha mchezaji mmoja, msimu huu bado hawajawa vyema sana lakini ngoma ya watani hiko huwa sio sababu kuu.

    Los blancos walio chini ya Benitez tumeona wakiwa na kiwango kizuri huku kocha huyo akifanya mabadiliko ya hapa na pale hasahasa safu ya ushambuliaji kwa kumchezesha Bale namba 10 kitu ambacho kimeonekana kuwa na manufaa zaidi kwa Benzema akiwa kama ndie mshambuliaji namba 9 na kwa sasa anamagoli 5 akiwa kinara sawa na Ronaldo.

    Unajua Benitez ni miongoni mwa makocha waliopita ligi nyingi kwa maana ni mtu anae jua kubadilika kimbinu dhidi ya timu ambayo anakutana nayo na ukiangaza mchezo huu dhidi ya watani wao ambapo mara nyingi wanacheza soka la undava halito mpa tabu sana.

    Kocha huyu Rafael tangu atue Santiago Bernabeu amekuwa anabadili wachezaji mara kwa mara na kati ya wachezaji 23 wa klabu hiyo tayari wachezaji 22 wamepata walau nafasi ya kucheza kulingana na uhitaji wa mchezo na kubadilika huko mara kwa mara imekuwa inatoa ugumu kwa mpinzani anaekutana nae.

    Kuna sare naiona kwenye mchezo huu ambao utawala wa mpira utakuwa kwa Real huku Simeone akishambulia kwa kustukiza kwa kumtumia Mfaransa Griezman na huenda akamuanzisha Torres ambae amekuwa anafanya vyema mbele ya Real.

    Upande wa Real nadhani chagizo ni ndelemo za Ronaldo kwa historia aliyo iandika Bernabeu kwa maana atahitaji kuendeleza moto wake wa kufunga .

      Kumbuka Real wanapoint 14 nafasi ya 3 na A.Madrid wana point 12 nafasi tano katika msimamo wa ligi.

    ::::::                           EVERTON VS LIVERPOOL

    The Merseyside derby

      Haya safari inamalizikia Uingereza katika Ligi kuu inayojulikana kama EPL sehemu ambayo imetanda giza nene kutokana na kushuka kwa viwango vya wachezaji wengi katika timu kubwa na kupelekea kufanya vibaya kwenye michuano ya Vilabu Barani Ulaya.

    Tukitupia jicho pale Jiji la Liverpool kutakuwa na sebene lililopoa kwa maana timu ya Liverpool na Everton hivi sasa wanaonekana kuwa na viwango vinavyo shabihana.

    Kiukweli hakuna wavumilivu kama mashabiki wa Liverpool lakini hakuna mzembe kama kocha wao Rogers kwa maana bado hajui cha kufanya mbele ya mashabiki wa Liverpool.

    Kiukweli amekuwa haeleweki katika maswala ya kutumia mifumo kulingana na wachezaji waliopo pia timu imekuwa haina muunganiko mzuri inapata matokeo kwa kubahatisha huku safu ya Ulinzi ikiwa kichocheo cha matokeo mabovu.

    Dhidi ya Everton Sturridge karejea na tunajua umuhimu wake na mchezo huu ndo atakuwa mwanga kwa Rogers .

    Everton wao hawatabiliki ingawa msimu huu walau wako vyema wakichagizwa na safu ya ushambuliaji inayo ongozwa na Kone pamoja na Lukaku.

    Mchezo lazima utakuwa wa kasi na timu zote zikishambuliana hapa na pale lakini matokeo yataamuliwa na safu za ulinzi kwa maana ya makosa ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa katika beki za timu hizi.

    Nakumbuka mara ya kwanza kabisa timu hizi zilipokutana ilikuwa ni 13/10/1894 hapo hata Tanganyika haitambuliki kwa jina hilo na mchezo huo Everton wakaibuka na ushindi wa goli 3-0 kisago kikubwa ni mwaka 1935 Liverpool akishinda goli 6-0 ila msimu uliomalizika mchezo wa mwisho tukashuhudia sare ya 0-0.

    Kumbuka wamesha kutana mara 224 kwa maana hiyo mchezo wa jumapili utakuwa wa 225 Liverpool wameshinda michezo 88 Everton akishinda michezo 66 na sare 70.

    Ni hayo ila kwa kiwango cha hivi sasa kuna kila dalili za Liverpool kuendelez kupotea kama hakuta fanyika mabadiliko maana tumekumbuka enzi zile za kina Ian Rush,Dixie Dean ngoja tusubiri ujuzi wa Milner na Barry wakipigania timu zao Everton nafasi ya 5 pointi 12 huku Liverpool nafasi ya 9 point 11.

    ::::
                            ARSENAL VS MANCHESTER UNITED


    Hapa bhana pana maneno mengi sana lakini pia kuna majigambo ya kila namna kwa mashabiki wa vilabu hivi ingawa upande mmoja huonekana kulemewa na kejeli za hapa na pale nawazungumzia mashabiki wa Manchester United majigambo yao kwa mashabiki wa Arsenal.

      Kumbuka kwa wewe mshabiki wa kati ya vilabu hivi  kwa mara ya kwanza kabisa timu hizi zilikutana 13/10/1894 kipindi hicho Manchester walijulikana kama Newton Heath na Arsenal wakitambulika kama Woolwich Arsenal na kwenye mchezo huo walitoka sare ya kufungana 3-3.

      Sasa timu hizi zimekutana mara 221 safari hii itakuwa mara 222 na mara hizo 221 Manchester United wameibuka na ushindi mara 93 Arsenal wakishinda mara  79 na tukashuhudia sare 49  kwa maana hiyo Arsenal anatafuta ushindi wa 80, Manchester United wanatafuta ushindi wa wa 94 au pengine tukashuhudia sare ya 50.

    Mchezo wa mwisho walipo kutana tulishuhudia sare ya 1-1 lakini kumbuka kipigo kikubwa zaidi pindi timu hizi zilipo kutana Arsenal alipokea kichapo cha goli 8-2 ilikuwa ni tarehe 28/8/2011 mchezo ambao umekuwa ukiwatesa sana mashabiki wa Arsenal mpaka leo.

    Ni mchezaji mmoja tu aliebaki ambae anauwezo wa kuboresha zaidi rekodi yake ya kufumania nyavu pindi timu hizi zikikutana si mwingine bali ni Rooney ambae mpaka sasa anagoli 9 akiwa kinara.

      Arsenal wapo nafasi ya 4 wakiwa na pointi 13 wakati Manchester United wapo kileleni kwa mara ya kwanza baada miaka 2 wakiwa na pointi 16.

    Sasa kuelekea katika mchezo huu ambao umekuwa na matokeo ya upande mmoja kwa maana hata kama Manchester United hawafanyi vyema basi pindi wakikutana na Arsenal kumekuwa na mteremko.

    Safari hii hali ya mambo ipo kinyume kwa maana katika misimu miwili Manchester United haikuwa vyema ukilinganisha na Arsenal lakini bado walikuwa na uhakika wa kupata matokeo mbele ya arsenal tunaona msimu huu kikosi cha Van Gaal licha ya kwamba bado kinatafuta ubora kama ule wa enzi ya Ferguson lakini wamekuwa na matokeo mazuri kuliko wapinzani wao kikosi cha Wenger ambacho bado hatuoni mabadiliko yoyote.

    Tunaiona Arsenal ambayo nafasi ya kiungo mkabaji ni tatizo na kumekuwa hakuna mawasiliano mazuri kati ya safu ya beki za kati na kiungo kwa maana hiyo pasipo marekebisho kwa kuangalia kiwango kizuri cha Martial na Mata tutazungumza mengine.

    Van Gaal kuelekea mchezo huu huku akiwa na kumbukumbu nzuri ya kutokufungwa na Arsenal katika mara mbili walizo kutana katika ligi nadhani marekebisho kwa upande wake ni katika beki kujisahau hapa na pale lakini kwa asilimia kadhaa anauwezo wa kupata matokeo mbele ya Arsenal.

    Miaka 19 ya Mzee Wenger licha ya mafanikio makubwa aliyo ipatia Arsenal lakini ''CV'' yake inashuka kwa kasi sana na kama atacheza kama ambavyo tumeishuhudia Arsenal ikicheza mpira mwingi pasipo kujilinda katika Uefa basi itakuwa dhahma kwa upande wake mbele ya Mashetani wekundu.

    Mpira sio historia kwa maana ya kuipa Manchester United ushindi lakini Arsenal wataamua matokeo yaweje kama watacheza kwa wimbi la Manchester hatuwawezagi basi itakula kwao mazima.

       Ni hayo tu ngoja tusubiri michezo hii ya kusisimua Jumapili hii.

    KWA MAONI NA USHAURI:

               choikangta.ckt@gmail.com

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: UCHAMBUZI YAKINIFU MECHI KUBWA SITA WIKENDI HII,EPL,BUNDESLIGA,LIGUE 1,LA-LIGA NA EREDIVISIE.......... Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top