Dar es Salaam,Tanzania.
KLABU ya Simba imeingia mkataba wa miaka miwili na kocha Mcameroon, Joseph Omog,huku ukimchimba mkwara kumtupia virago vyake, endapo atashindwa kuipatia mafanikio
timu hiyo.
Rais wa Simba, Evans Aveva aliyasema hayo baada ya kuingia mkataba wa miaka miwili na kocha huyo.
Omog aliwahi kuifundisha Azam FC na ndiye aliyeipatia timu hiyo ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba jana ilimtambulisha rasmi kocha huyo aliyewasili nchini juzi usiku na kusaini mkataba huo wa miaka miwili.
Aveva alisema kuwa anaamini Omog atafanya vizuri na kitendo chao cha kutimua timua makocha kina lengo la kumpata atakayeiinua timu hiyo na kufanya vizuri katika LigiKuu.
Alisema kuwa hata Omog atatupiwa virago mara moja endapo atashindwa kuipatia mafanikio Simba.
Akizungumza baada ya kutia saini, Omog alisema yeye haogopi kutimuliwa kwani hiyo ni sehemu ya kazi ya makocha.
Alisema Simba ni timu nzuri na atajitahidi kuendana na mfumo wao, ambapo alitamba kuiwezesha kufanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzana Bara msimu ujao na mashindano mengine. Alisema anataka kwanza kuona viwango vya wachezaji ili ajue anahitaji kufanya nini kukiboresha kikosi chake na atasajili wachezaji gani.
Uongozi wa Simba umempa nafasi kocha huyo kusaka wasaidizi wake anaowataka ili kumwezesha kufanya kazi yake vizuri.
Kwa kauli hiyo kocha aliyeiwezesha Simba kumaliza ya tatu katika msimu uliopita wa ligi, Mganda Jackson Mayanja ameachwa rasmi na klabu hiyo.
Amog aliongeza kusema kuwa anajua Simba ina kiu ya mataji, ambapo aliahidi kuhakikisha msimu ujao inatwaa ubingwa na kufuzu kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
Simba zaidi ya misimu mitatu imeshindwa kufuzu kwa mashindano ya kimataifa baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Aidha,
Patrick Kahemela ametambulishwa rasmi kuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, ambapo ameomba kuungwa mkono ili kufanikisha majukumu yake.
Alisema Simba ina wachama wengi na inaweza kujitegemea kwa kuwatumia wanachama hao.
Simba itakuwa klabu ya pili kwa Omog kufundisha Tanzania baada ya awali kuwa na Azam FC, aliyoiongoza kwa msimu mmoja na nusu ikishinda mechi 30 kati ya 55 za mashindano yote, sare 14 na kufungwa 11.
Kocha huyo aliyeipa Leopard FC ya Congo Brazaville Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2014, enzi zake alichezea Yaounde na ni mwalimu wa kiwango cha juu cha ufundishaji soka na mazoezi ya viungo.
0 comments:
Post a Comment