Kocha wa timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars Charles Mkwasa anasema wachezaji wake wako tayari kuikabili Nigeria katika mchuano wa mwishoni mwa wiki hii kufuzu katika fainali ya mataifa bingwa barani Afrika mwaka 2017 nchini Gabon.
Tanzania itakuwa mwenyeji wa Nigeria siku ya Jumamosi katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.
Vijana wa Taifa Stars kwa muda wa wiki moja iliyopita wamekuwa wakipiga kambi nchini Uturuki na walicheza mchuano wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Libya na kufungwa mabao 2 kwa 1.
Kocha Mkwasa ameiambia tovuti ya Shirikisho la soka TFF kuwa kambi hiyo imewasaidia vijana wake kujiamini na sasa wako tayari kumenyana na mabingwa hao wa zamani wa soka barani Afrika.
Aidha, amesifia mazingira ya kambi yao nchini Uturuki na kusisitiza imewapa mazingira ya kujiimarisha zaidi na wanakamilisha kambi yao siku ya Jumatatu kabla ya kurejea nyumbani kuisubiri Nigeria.
Tanzania ipo katika kundi moja na Misri pamoja na Chad.
Mchuano wa kwanza wa makundi Tanzania wakicheza wakiwa ugenini walifungwa na Misri mabao 3 kwa 0.Kibarua cha Jumamosi kitakuwa kipimo cha Mkwasa ambaye alichukua mikoba ya Mart Nooij kutoka Uholanzi aliyefutwa kazi mwezi Juni.
0 comments:
Post a Comment