Dar es Salaam. Klabu ya soka Yanga imewazuia nyota wake kujiunga na kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars na badala yake wachezaji wote wa kikosi hicho waliondoka jana kwenda Tukuyu Mbeya kuweka kambi.
Yanga iliondoka jana kwenda Mbeya kuweka kambi ili kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam utakaofanyika Agosti 22 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hata hivyo, kuna hatihati pia wachezaji wa Azam nao huenda wasijiunge na Taifa Stars kwani waliondoka jana kwenda Zanzibar kuweka kambi kujiandaa mchezo huo dhidi ya Yanga.
Hali hiyo inaweza kumpa wakati mgumu kocha wa muda wa Taifa Stars ambaye pia ni kocha msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa anayetaka kukiandaa kikamilifu kikosi chake kwa ajili ya mchezo wa kufuzu kwa Mataifa ya Afrika dhidi ya Nigeria mwezi ujao.
Yanga imetoa wachezaji wanane kwenye kikosi cha Stars chenye wachezaji 29 kilichoitwa wiki hii na kocha Mkwasa wakati Azam imetoa wachezaji tisa, huku kambi ya Stars inatarajia kuanza leo jijini Dar es Salaam.
Wachezaji wa Yanga walioitwa Stars ni; Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Salum Telela, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Deus Kaseke, Simon Msuva na Ali Mustapha.
Stars itaweka kambi Dar es Salaam kwa wiki mbili na Agosti 23 itapanda ndege kwenda Uturuki katika kambi nyingine itakayohusha michezo ya kirafiki dhidi ya Libya na Kuwait.
Yanga iliondoka jana asubuhi kwa basi kwenda Tukuyu Mbeya na leo itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Kimondo FC ya Mbozi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba alisema wao wana programu tofauti na timu nyingine na hawezi kuzungumzia suala hilo kama watawaruhusu wachezaji wao au hawatawaruhusu na kila kitu kitajulikana leo.
Kwa upande wa Yanga inaelezwa kuwa katibu mkuu wa klabu hiyo, Dk Jonas Tiboroha amegoma kuruhusu wachezaji wa timu hiyo kujiunga na Stars kwa madai kuwa watakuwa kambini Tukuyu.
0 comments:
Post a Comment