London, Uingereza.
MWAMUZI Mark Clattenburg ameteuliwa kuchezesha mchezo wa Jumamosi hii wa wapinzani wa jadi wa jiji la Manchester,Manchester United na Manchester City utakaochezwa katika dimba la uwanja wa Old Trafford.
Clattenburg,41,ambaye kwa sasa ndiye mwamuzi bora zaidi nchini Uingereza na barani Ulaya amepewa jukumu hilo leo Jumatatu ikiwa ni mara ya tatu mfululizo anapewa rungu kuiamua miamba hiyo iliyouanza msimu mpya wa ligi kwa kushinda michezo yao mitatu ya mwanzo.
Aidha katika mchezo huo unaotarajiwa kuwa utakuwa na ushindani wa aina yake,Clattenburg, atakuwa akisaidiwa na Jake Collins pamoja na Steve Bennett huku kamisaa akiwa Mike Dean.
Msimu uliopita Clattenburg aligonga vichwa vya habari duniani baada ya kuteuliwa kuchezesha fainali tatu kubwa.Alianza kwa kuchezesha fainali ya kombe la FA akaja fainali ya ligi ya Mabingwa Ulaya kisha akafunga kazi kwa kuchezesha fainali ya Euro 2016 iliyoisha kwa Ureno kutawazwa mabingwa kwa kuwabwaga wenyeji Ufaransa kwa bao 1-0 lililofungwa na Elder dakika za majeruhi.
0 comments:
Post a Comment