728x90 AdSpace

  • Latest News

    Monday, September 19, 2016

    MAKALA :MKWASA MIMI NIMEKUELEWA SIJUI TFF NA VILABU


    Na Paul Manjale.

    WASWAHILI husema utavuna ulichopanda.Hii ina maana,ukipanda mahindi tegemea kuvuna mahindi. Vivyo hiyo hata ukipanda mihogo tegemea kuvuna mihogo na siyo vinginevyo.

    Hata hivyo,mavuno pia yanategemea na mahali ulipopanda, ukipanda kwenye vichaka au mawe ni lazima mavuno yawe hafifu au ukose kabisa.Hivyo ili kila kitu kiende sawa na kwa wakati, ni lazima kanuni zifuatwe tena kwa ufasaha wa hali ya juu.

    Majuzi timu yetu ya taifa,Taifa stars,ilishindwa kufuzu michuano ya AFCON baada ya kumaliza kampeni zake ikiwa mkiani mwa kundi G nyuma ya Misri iliyofuzu na Nigeria iliyoshika nafasi ya pili.

    Mengi yamesemwa kuhusu kushindwa huko kwa Stars, lakini ukweli unabaki pale pale kuwa Tanzania tumevuna tulichokipanda.Tumepanda kushindwa,tumevuna kushindwa.

    Kocha Mkuu wa Taifa Stars,Charles Mkwasa ameweka bayana sababu za kufanya vibaya kwa timu hiyo. Amesema kufanya vibaya kumechangiwa na vilabu kushindwa kuwaandaa  vizuri wachezaji wao hali inayofanya wawe lege lege na washindwe

    kuhimili mchezo kwa dakika tisini.

    Sababu nyingine aliyoitoa Mkwasa na nikamuelewa zaidi pengine kuliko ile ya kwanza ni nchi kuwa na ligi mbovu na isiyo na ushindani unaokidhi haja.Maandalizi ya kuunga unga kwa timu ya taifa pamoja na Programu zisizotekelezeka.

    Vilabu kushindwa kuwaandaa vizuri wachezaji wao!!

    Wachezaji kuwa legelege ni matokeo ya vilabu kushindwa kuwapa wachezaji wao mazoezi ya kutosha ambayo yatawajengea stamina na kuwapa pumzi ya kuhimili mikimiki uwanjani.Pengine mazoezi ya siku hizi yamejaa zaidi maongezi/mazungumzo kuliko vitendo.

    Ligi mbovu na isiyo na ushindani unaokidhi haja!!

    Ligi yetu ni mbovu imejaa mambo mengi ya ajabu ajabu.Waamuzi kuchezesha kwa upendeleo,panga pangua ya ratiba,ligi kusimama muda mrefu bila ya sababu za msingi,rufaa zisizopatiwa ufumbuzi wa haraka.Migogoro.Vilabu kushindwa kutoa ushindani wa kweli.Rushwa,upangaji wa matokeo na kadhalika.

    Hakika tukiendelea kutegemea ligi hii tuliyonayo sasa ili tuwe na timu bora ya taifa,hatutakuwa na tofauti na mkulima anayepanda mbegu zake juu ya mawe kwani hatavuna chochote hata kama atakuwa akimwagilia maji usiku na mchana.Zaidi atakuwa akipoteza nguvu na muda wake.

    Programu zisizotekelezeka.

    Kama unakuwa na makocha harafu unashindwa kutekeleza programu zao kwa visingizio visivyo na tija ni dhahiri kuwa umekubali kuwa sawa na mkulima anayepokea ushauri wa mabwana/mabibi shamba na kuufungia kabatini asiufanyie kazi harafu akategemea kupata mavuno mazuri.

    Tukumbuke timu bora ya taifa haipatikani kwenye ligi iliyojaa migogoro na rufaa zisizokwisha.Timu bora ya taifa haipatikani kwenye ligi ambayo ushindi unanunuliwa.Timu bora ya taifa haipatikani kwenye ligi ambayo ratiba inapanguliwa hata kabla ya ligi husika haijaanza.Timu bora ya taifa haipatikani katika nchi ambayo programu za makocha hazitekelezeki.

    Ukiona timu za taifa zinakuwa nzuri jua zimetoka katika nchi ambazo mpira wake unaendeshwa kisayansi.Hakuna maandalizi ya kuunga unga.Hakuna panga pangua ya ratiba,hakuna longo longo katika utekelezaji wa programu za makocha na kadhalika.

    Anachokimaanisha Mkwasa hapa ni kwamba hakuna miujiza itakayoiokoa Taifa Stars na aibu zaidi ya maandalizi makini,programu zinazotekelezeka pamoja na ligi bora vinginevyo tutaendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu miaka nenda rudi.

    Mimi nimemuelewa Mkwasa hebu na nyinyi mueleweni bhasi ili mambo yaende sawia kama kwa wenzetu Uganda ambao wamefuzu AFCON baada ya kusubiri kwa miaka 38.  


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: MAKALA :MKWASA MIMI NIMEKUELEWA SIJUI TFF NA VILABU Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top