Turin,Italia.
ARSENAL imechesha tena katika mbio za kutaka kumsajili mshambuliaji wa Argentina,Gonzalo Higuain,hii ni baada ya staa huyo wa Napoli kukubali kutua Juventus kwa kandarasi ya miaka minne.
Mapema wiki hii kuliibuka habari kuwa Arsenal ilikuwa tayari kutoa €50m pamoja na mshambuliaji wake,Olivier Giroud (29),ili kumpata Higuain (28) lakini taarifa za ndani toka Italia zinasema tayari Juventus imeshafikia makubaliano binafsi na Higuain aliyefunga mabao 36 katika michezo 35 msimu uliopita.
Katika makubaliano hayo Juventus itakuwa ikimlipa Higuain mshahara wa €7.5m kwa mwaka ambao ni ongezeko kubwa zaidi kutoka katika mshahara anaolipwa na Napoli kwa sasa.
Taarifa zinazidi kutanabaisha kuwa ili kuhakikisha kuwa Dili hilo linakamilika haraka,wakuu wa bodi ya Juventus wako tayari kutoa kitita cha €75m na mchezaji mmoja kati ya Simone Zaza, Daniele Rugani,Stefano Sturaro ama Roberto Pereyra ili kufikia dau la €94m linalotakiwa na Napoli.
Ikiwa Juventus itafanikiwa kukamilisha dili hilo hii itakuwa ni mara ya pili kwa Arsenal kumkosa mshambuliaji huyo wa zamani wa Real Madrid.Mara ya kwanza ilikuwa ni miaka mitatu iliyopita pale ilipozidiwa ujanja dakika za mwisho na Napoli.
0 comments:
Post a Comment