Ratiba ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation
Cup) imetolewa leo, ambapo jumla ya timu 16 zinakutana katika hatua hiyo
(16 bora) itakayoanza kutimua vumbi wikiendi ya Februari 26-1 Machi
2015 katika viwanja mbalimbali nchini.
Michuano hiyo iliyoshirikisha jumla ya timu 64 kutoka ngazi za Ligi
Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili, inaingia katika
mzunguko wa nne huku kukiwa na timu kutoka katika ngazi zote za ligi za
TFF nchini.
Ijumaa tarehe 26 Februari kutachezwa michezo miwili ambapo, Ndanda FC
watawakaribisha JKT Ruvu katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini
Mtwara, huku Coastal Union wakiwa wenyeji wa wakata miwa wa Mtibwa Sugar
katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Jumamosi, Februari 27, Mwadui FC watawakaribisha Rhino Rangers katika
uwanja wa Mwadui Complex - Shinyanga, Jijini Mbeya Tanzania Prisons
watacheza na mshindi kati ya Mbeya City/Wenda FC kwenye uwanja wa
Sokoine jijini Mbeya.
Februari 28, michezo mitatu itachezwa, Simba SC watawakaribisha
Singida United katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Panone FC
watacheza dhidi ya Azam FC uwanja wa Ushirika mjini Moshi, huku Toto
African wakicheza na wachimba madini wa Geita Gold katika uwanja wa CCM
Kirumba jijini Mwanza.
Raundi hiyo itamalizika Machi 01, 2015 kwa mchezo mmoja kuchezwa
ambapo Young Africans watawakaribisha JKT Mlale katika uwanja wa Taifa
jijini Dar es salaam.
Bingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation
Cup) mwaka huu ataiwakilisha Tanzania kwenye Mashindano ya kombe la
Shirikisho Barani Africa (CAF CC) mwakani 2017.
0 comments:
Post a Comment