Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi ya Ligi (Kamati ya Saa 72) imekutana jana (Februari 16, 2016) kupitia taarifa za mechi mbili za Kundi C la Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes kati ya JKT Kanembwa na Geita Gold SC, na Polisi Tabora na JKT Oljoro ambapo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilisimamisha matokeo yake hadi taarifa hizo zitakapopitiwa.
JKT Kanembwa ilifungwa mabao 8-0 na Geita Gold SC katika mechi iliyofanyika Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, wakati Polisi Tabora ilishinda mabao 7-0 dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Baada ya kupitia taarifa hizo na vielelezo vingine, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeonyesha mashaka kutokana na kuwepo viashiria vya upangaji wa matokeo (match fixing).
Kwa vile suala hilo linahusisha masuala ya kinidhamu, na kwa kuzingatia Ibara ya 50(1) na (11) ya Katiba ya TFF na Ibara ya 69 ya Kanuni za Nidhamu za TFF, Kamati ya Saa 72 imemuelekeza Katibu Mkuu wa TFF apeleke suala kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya uchunguzi na hatimaye kufanya uamuzi.
0 comments:
Post a Comment