Kiungo mkongwe wa Simba, Mwinyi Kazimoto anatuhumiwa kumpiga
mwandishi wa habari, hali iliyosababisha afikishwe katika kituo kikuu cha
Polisi cha Shinyanga.
Kazimoto amefikishwa katika kituo hicho kilicho karibu
kabisa na hospitali ya mkoa wa Shinyanga kwa madai ya kumshambulia mwandishi wa
gazeti la Mwanaspoti, Mwanahiba Richard.
Imeelezwa, Kazimoto alimshambulia Mwanahiba baada ya mazoezi
ya Simba yaliyofanyika katika Uwanja wa Kambarage ulio katika eneo la Majengo
mjini Shinyanga, jana.
Mara baada ya mazoezi, inadaiwa Kazimoto aliyechipukia
kisoka mkoani Mwanza, alimvamia alimvamia Mwanahiba na kumpiga akidai aliandika
stori kwamba kiwango chake pamoja na wachezaji wengine katika mechi mbili za
Mbeya City, pia Prisons ya Mbeya hakikuwa kizuri na wanapaswa kuchunguzwa.
Kazimoto alionekana kutofurahishwa na habari hiyo
iliyoonekana ni kama tuhuma, hivyo kupandwa na hasira hadi kuingia katika
mgogoro huo na Mwanahiba.
Inadaiwa baada ya kipigo hicho, Mwanahiba aliriripoti katika
kituo hicho cha polisi na kupewa hati mashitaka (RB) yenye yenye namba
SHY/RB/895/2016, fomu ya matibabu (PF3) kisha akapelekwa hospitali kwa
matibabu.
Kazimoto hakupatikana kulizungumzia suala hilo, pia hakuna
kiongozi wa Simba aliyelizungumzia, huku kukiwa na hekaheka ya kutaka
kulimaliza kwa amani jambo ambalo linaonekana kupingwa na upande wa
wanaolalamika.
Kwa upande wake Mwanahiba, alisema aliandika stori iliyokuwa
ikieleza viongozi wa Simba kutoridhishwa na baadhi ya wachezaji wa Simba akiwemo
Kazimoto baada ya wao kupoteza mchezo kwa kufungwa na Prisons kwa bao 1-0
mjini Mbeya katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.
"Ilikuwa ni stori ya mwaka jana, leo Kazimoto akaniita
na kuanza kuniuliza akitaka nimwambie kiongozi gani aliyeniambia. Nikamueleza
si kazi yake, kifupi niliandika na anajua kama hilo lilitokea.
"Alipoona nimemzidi hoja, akaanza kunidhambulia kwa
ngumi na mateke. Akanipiga hadi aliponiumiza kichwani, wakati huo wenzake
walikuwa kwenye basi wanashuhudia, ndiyo Mgosi akawahi kushuka na
kuniokoa," alisema Mwanahiba.
Lakini Mhariri wa Mwanaspoti, Michael Momburi amesema suala
hilo linashughulikiwa.
"Kweli hilo suala lipo, limefikishwa polisi na sisi
tunaendelea kufuatilia. Hakika si suala sahihi na halifurahishi na tayari
tumelikabidhi suala hilo kwa mwanasheria wa kampuni analishughulikia kwa
kushirikiana na RPC wa Shinyanga," alisema Momburi.
0 comments:
Post a Comment