Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo limetangaza viingilio
vya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) Jumamosi kati ya watani wa jadi
Simba SC dhidi ya Yanga SC utakaochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es
salaam, huku kiingilio cha chini kikiwa ni Shilingi elfu saba tu
(7,000).
Kiingilio cha juu cha mchezo huo kitakua shilingi Elfu Thelathini
(30,000) kwa VIP A, Elfu Ishirini (20,000) VIP B & C, Elfu Kumi
(10,000) kwa viti vya rangi ya machungwa (Orange), na Elfu Saba (7,000)
kwa viti vya rangi ya bluu na kijani.
Tiketi za mchezo huo zitaanza kuuzwa siku ya Ijumaa saa 2 kamili
asubuhi katika vituo vya TFF (Karume), Buguruni Olicom, Ubungo Oilcom,
Kidongo Chekundu (Mnazi Mmoja), Posta (Agip), Dar Live (Mbagala), Uwanja
wa Taifa, Makumbusho Stand, Kivukoni Ferry.
Mchezo huo utachezeshwa na waamuzi wote wenye beji za FIFA, mwamuzi
wa katikati Jonesia Rukyaa (Kagera), akisaidiwa na Josephat Bulali
(Tanga), Samwel Mpenzu (Arusha), mwamuzi wa akiba Elly Sasii (Dar) huku
Kamisaa wa mchezo huo akiwa Khalid Bitebo (Mwanza).
Ligi hiyo ya Vodacom itaendelea Jumamosi kwa michezo sita, Young
Africans v Simba (Taifa), Mbeya City v Azam (Sokoine), Stand United v
JKT Ruvu (Kambarage), Toto Africans v Kagera Sugar (CCM Kirumba), Mgambo
Shooting v Tanzania Prisons (Mkwakwani) na Majimaji FC v Mtibwa Sugar
(Majimaji).
Jumapili ligi hiyo itaendelea kwa michezo miwili, Mwadui FC v Coastal
Union uwanja wa Mwadui Complex, huku Ndanda FC wakicheza dhidi ya
African Sports uwanja wa Nagwanda Sijaon mjini Mtwara.
0 comments:
Post a Comment