WAPINZANI wa jadi nchini, Simba na Yanga wanatarajia kukutana katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ifikapo Septemba 26 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini jana zinasema kuwa mchezo huo utakuwa ni wa raundi ya nne ya Ligi hiyo inayotarajiwa kuanza Septemba 12 mwaka huu na itashirikisha timu 16 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.
Taarifa zaidi kutoka katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zinaeleza kuwa mabingwa watetezi wa ligi hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Simu za Mikononi ya Vodacom, Yanga wataanza kampeni ya kutetea ubingwa wanaoushikilia kwa kuwakaribisha Coastal Union kutoka Tanga.
Chanzo hicho kiliendelea kusema kwamba Simba ambayo ni maarufu kwa jina la Wekundu wa Msimbazi wenyewe wataanzia ugenini kwa kucheza na African Sports ya Tanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini humo.
"Mechi ya Simba na Yanga imepangwa kufanyika Septemba 26 na Yanga wataanzia Dar wakati Simba itaanzia Tanga", alisema mmoja wa viongozi wa juu wa klabu hizo mbili.
Hata hivyo chanzo hicho kiliongeza kuwa, klabu zinazoshiriki ligi hiyo zilikabidhiwa nakala ya ratiba juzi Jumatatu na baadhi yao walihitaji kubadilishiwa baadhi ya michezo ya awali na hiyo inatokana na changamoto za usafiri.
Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, hakuwa tayari kusema lini shirikisho hilo litatangaza rasmi ratiba hiyo ya ligi.
"Nadhani tutatoa wiki hii", Mwesigwa alisema.TFF kupitia Kamati ya Mashindano ililazimika kufanya mabadiliko kwenye ratiba baada ya ile ya awali iliyopangwa ilikuwa inaonyesha Ligi Kuu ya Bara itaanza Agosti 22 lakini ililazimika kusogezwa mbele kwa kuangalia maslahi ya timu ya Taifa (Taifa Stars).
Ligi hiyo ambayo inatoa wawakilishi wa nchi katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, itatanguliwa na mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Azam utakaofanyika Jumamosi Agosti 22 mwaka huu jijini.
Msimu ujao wa mwaka 2015/ 2016 unatarajiwa kushirikisha timu 16 wakati nne zilizopanda daraja ni pamoja na African Sport, Majimaji ya Ruvuma, Mwadui (Shinyanga) na Toto Africans ya Mwanza.
0 comments:
Post a Comment