Mlandizi,Pwani.
UONGOZI wa timu ya soka ya Ruvu Shooting,jana Jumatatu, Juni 12, 2017 ulikutana chini ya mwenyekiti wake Kanali wa Jeshi,Mkuu wa Kikosi cha Jeshi (CO) 832, Ruvu JKT Charles Mbuge, pamoja na mambo mengine kujadili taarifa ya mwalimu Malale Hamsini Keya aliyoiwasilisha baada ya kumalizika kwa msimu wa ligi 2016/17.
Kwa ushauri na mapendekezo ya mwalimu,uongozi umeamua kuachana na wachezaji 10 kwasababu mbalimbali, lakini pia kuanza mchakato wa kusajili wachezaji wengine wasiopungua tisa kutokana na ushauri na mapendekezo ya benchi la ufundi.
Wachezaji sita kati ya 10 walioachwa ni kipa Elias Emanuel ambaye alicheza mechi moja msimu mzima dhidi ya Mbao fc na kufungwa goli nne, Ismail Mgunda ambaye alicheza mechi nane, baadaye akatoroka kambini,mpaka sasa haijulikani alipo na Richard Peter ambaye hakucheza mechi hata moja kutokana na kiwango chake cha uchezaji kuwa cha chini sana kulinganisha na wechezaji wengine.
Wengine walioachwa ni Claide Luita ambaye alicheza michezo mitatu mzunguko wa kwanza, mzunguko wa pili hakucheza mchezo hata mmoja baadaye aliamua kuondoka mwenyewe ingawa kocha Malale kamsifia kwa kipaji na ubora wa kucheza mpira, Amour Bakari aliyecheza mchezo mmoja tu kutokana na uwezo na maumivu ya mara kwa mara na Alex Sety ambaye alicheza michezo sita.
Wachezaji wengine wanne walioachwa watatajwa baadaye baada ya taratibu na
maelezo kuhusu ushiriki wao katika timu kukamilika.
Wachezaji tisa wanaotakiwa kusajiliwa ni beki wa kati mmoja, viungo wa pembeni wawili,viungo wakabaji wawili, full back wa kulia mmoja na washambuliaji watatu.
Kikosi kazi cha viongozi wanne kwa ushirikiano na walimu wa timu tayari kimeanza kazi ya usajili kazi inayofanywa kimyakimya, kwa usahihi sana mithili ya sumu ya nyoka Kifutu.
0 comments:
Post a Comment