Moscow,Urusi.
MABAO mawili ya kipindi cha pili ya kiungo Arturo Vidal na mshambuliaji Eduardo Vargas yameipa Chile ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya mabingwa wa Afrika Cameroon katika mchezo wa kwanza wa kundi B wa michuano ya kombe la mabara uliochezwa kwenye uwanja wa Otkrytiye Arena huko Moscow,Urusi.
Shujaa wa mchezo wa leo kwa upande wa Chile alikuwa ni staa wa Arsenal, Alexis Sanchez aliyepika mabao yote mawili muda mfupi baada ya kuingia uwanjani akitokea benchi.
Sanchez aliyekuwa akisumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu alianza kuipa wakati mgumu Cameroon baada ya pasi yake ya juu kutua kichwani kwa Arturo Vidal na kuifungia Chile bao la kwanza katika dakika ya 81.
Eduardo Vargas aliihakikishia Chile pointi zote tatu baada ya kuifungia bao la pili katika dakika ya 93 ya mchezo baada ya kuunasa mpira uliopigwa na Sanchez na kupanguliwa na kipa wa Cameroon,Fabrice Ondoa.
Aida katika mchezo huo ilishuhudiwa bao la kipindi cha kwanza la Eduardo Vargas likikataliwa kwa madai kuwa alikuwa ameotea huku lile la pili likikubaliwa baada ya mwamuzi wa kati kuhitaji msaada wa teknolojia ya VAR ili kufanya maamuzi.
0 comments:
Post a Comment