Dar Es Salaam,Tanzania.
Mahakama ya Kisutu ya jijini Dar Es Salaam imewanyima dhamana Rais wa mabingwa wa kombe la shirikisho Tanzania,Simba SC,Evans Aveva pamoja na Makamu wake Geoffrey Nyange Kaburu baada ya kuwakuta na makosa matano ya matumizi mabaya ya madaraka yao ikiwemo kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu.
Kati ya makosa hayo matano,matatu (3) hayana dhamana hii ina maana kwamba viongozi hao waliotiwa nguvuni tangu jana Jumatano watakaa mahabusu mpaka Julai 13 mwaka huu ambapo kesi yao itasomwa kwa mara nyingine.
Wawili hao walikatamatwa jana Jumatano na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa uchunguzi juu ya tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutokana na mauzo ya mchezaji raia wa Uganda,Emmanuel Okwi.
Inadaiwa kulikuwa kuna udanganyifu katika mauzo ya mchezaji Emmanuel Okwi kwenda klabu ya Esperance ya Tunisia kwamba kiasi kilichotajwa cha dola za Kimarekani 300,000, zaidi ya Sh. Milioni 600 si ambacho Simba ilipata katika biashara hiyo.
Taarifa zinasema Simba ilipata fedha zaidi kwenye biashara hiyo iliyochukua muda mrefu kukamilika, lakini katika kumbukumbu za klabu ikaandikishwa dola 300,000 tu.
0 comments:
Post a Comment