Amsterdam,Uholanzi.
WINGA wa zamani wa Manchester United ambaye kwa sasa anatesa na klabu yake mpya ya Olympique Lyon,Mholanzi Memphis Depay ameamua kuliweka soka pembeni kwa muda na kugeukia muziki.
Depay pamoja na mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya Uholanzi, Quincy Promes anayeichezea Spartak Moscow ya Urusi wameamua kuutumia muda wao wa mapumziko ya msimu kuandaa kibao matata cha muziki wa kufoka foka maarufu kama Rap.
Kibao hicho ambacho jina lake bado limefanywa siri kitakuwa katika lugha mbili za Kidachi (Kiholanzi) na Kiingereza na kitambulishwa Ijumaa ya wiki hii.
Tayari kipande kifupi cha video ya kibao hicho kimeshawekwa kwenye mtandao wa You Tube ambacho kinawaonyesha Depay na Promes wakiwa wamejinakshi kwa magari makali,vito vya thamani pamoja na mavazi ya bei mbaya.
Kuingia kwenye muziki kwa nyota hao wawili ni muendelezo wa kile ambacho kilishawahi kufanywa na nyota wengine wa Uholanzi kama vile Ryan Babel aliyewahi kuichezea Liverpool pamoja na Royston Drenthe aliyewahi kuvichezea vilabu vya Real Madrid na Everton.
0 comments:
Post a Comment