Osijek,Croatia.
KIUNGO nyota wa Real Madrid,Luka Modric anafanyiwa uchunguzi na mamlaka za juu za nchini kwao Croatia kwa kosa la kutoa ushahidi wa uongo mahakamani.
Modric mwenye umri wa miaka 31 anatuhumiwa kuizingia chaka mahakama ya Osijek County Court kwa kutoa ushahidi wa uongo kwenye kesi ya ukwepaji kodi na udanganyifu inayomhusu Meneja wake wa zamani,Zdravko Mamic.
Mamic,Mkurugenzi wa zamani wa klabu ya Dinamo Zagreb na mtu mwenye nguvu kubwa kwenye soka la Croatia anakabiriwa na kesi ya kuisababishia klabu hiyo hasara ya zaidi ya Pauni Milioni 13.
Mamic pamoja na kaka yake, Zoran Mamic na watu wengine wawili wanadaiwa kuwa walikuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa,ukwepaji kodi pamoja na udanganyifu katika masuala ya uuzaji wa wachezaji.
Mamic anadaiwa kuwa alijipatia fedha nyingi kupitia mauzo ya wachezaji ikiwemo Modric aliyeihama Dinamo Zagreb mwaka 2008 na kujiunga na Tottenham.
Inasemekana Mamic alifanya udanganyifu kwenye nakala za mauzo ya Modric na kujipatia fedha nyingi kuliko klabu ya Dinamo Zagreb iliyokuwa ikimmiliki mchezaji huyo.
Modric anadaiwa kuwa Juni 13 mwaka huu alitoa ushahidi ambao unapingana na ule aliowahi kuutoa hapo nyuma juu ya uhamisho wake kwenda Tottenham.
Modric alidai kuwa Julai 2004 aliingia makubaliano kuwa atapewa nusu ya fedha itakayopatikana katika mauzo yake lakini taarifa za waendesha mashitaka zinadai kuwa makubaliano hayo yalifanyika mwaka 2008 baada ya kuwa tayari ameshaihama Dinamo Zagreb.
Waendesha mashitaka hao pia wamedai kuwa mwaka 2015,Modric aliwaambia wapelelezi kuwa makubaliano hayo yalifanyika yeye akiwa tayari ameshauzwa kwenda Tottenham.
Kwa mujibu wa sheria za kimahakama za Croatia ni kwamba ikiwa itabainika kuwa Modric ameidanganya mahakama kwa makusudi ili kumlinda Mamic basi atakabiriwa na kifungo cha kuanzia miezi sita mpaka miaka mitano jela.
0 comments:
Post a Comment