Turin,Italia.
ISIWE SHIDA!!Klabu ya Juventus imekubali kuachana na mlinzi wake wa kulia,Dani Alves ili akatimize ndoto ya kuungana kwa mara nyingine na Kocha wake wa zamani Pep Guardiola ambaye kwa sasa anainoa Manchester City.
Juventus imefikia uwamuzi huo baada ya Alves kuomba kuondoka Turin licha ya kwamba bado ana mwaka mmoja kwenye mkataba wake wa sasa wa miaka miwili na miamba hiyo ya soka nchini Italia.
Alves ,34, alijiunga na Juventus Julai mwaka jana akitokea Barcelona kwa mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza mmoja zaidi lakini ameamua kuichenjia klabu hiyo ili akaungane tena na Guardiola aliyewahi kufanya nae kazi kwa miaka minne.
Taarifa za awali zinasema tayari Alves alishakubali kujiunga na Manchester City kwa mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya £8.6m.
Bado haijafahamika kama Juventus itataka fidia kutoka na kubariki kuondoka kwa Alves ama itaamua kumwachia huru mlinzi huyo anayetokea nchini Brazil ikiwa tu ataamua kusamehe mishahara yake yote aliyopaswa kulipwa kwenye mkataba wake uliosalia.
Ikiwa uhamisho huo utakamilika Alves atakuwa mchezaji wa tatu kujiunga na Manchester City tangu kufungiliwa kwa dirisha la usajili barani Ulaya baada ya kiungo Bernardo Silva aliyetokea Monaco na mlinda mlango Ederson Moraes aliyetokea Benfica.
Guardiola anataka kukamilisha usajili wa nyota wapya kabla ya kuanza kwa ziara ya kujiandaa na msimu mpya ili apate muda wa kutosha wa kukinoa kikosi chake ambacho kilishindwa kutwaa taji lolote msimu uliopita.
0 comments:
Post a Comment