Dar Es Salaam,Tanzania.
KOCHA wa timu ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17
Serengeti Boys, Bakari Shime ameahidi kuiadhibu Congo -Brazzaville
katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa
vijana utakaofanyika keshokutwa.
Akizungumza jana Shime alisema haangalii umri wa wapinzani wao bali anachoangalia ni uwezo wao.Alisema kuwa kikosi chake kimejiandaa vya kutosha wachezaji wake wana
ari na kwamba anatarajia ushindi wa kishindo katika mchezo huo ambao
watahakikisha wanatumia vyema uwanja wa nyumbani.
Serengeti ambayo iliweka kambi ya siku 10 Shelisheli na kurejea
mapema jana itashuka dimbani keshokutwa kwenye Uwanja wa Uhuru mchezo wa
kuwania kufuzu fainali za Afrika zitakazofanyika Madagascar mwakani.
“Kikosi changu hakina majeruhi, kambi imetupa uzoefu mkubwa wa
kupambana na vijana wa Congo-Brazzaville kwani nimewapa mbinu za kutosha
na kurekebisha kasoro ambazo zilijitokeza katika mchezo wetu na Afrika
Kusini."
Alisema katika mchezo huo ingawa Serengeti ilishinda mabao 2-0 kikosi
chake kilikua na upungufu hasa kwa washambuliaji wake ambao walipoteza
nafasi nyingi za wazi na kwamba iwapo wangezitumia vizuri wangefunga
mabao ya kutosha. Katika kambi hiyo, Serengeti ilijipima na Northern
Dynamo na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
“Tunahitaji sapoti kutoka kwa Watanzania, sio Serengeti Boys inacheza
bali Watanzania wanacheza hivyo tunahitaji sapoti kubwa katika mchezo
wetu wa Jumapili dhidi ya Congo-Brazzaville,” alisema Shime.
“Historia inaonesha mara nyingi Congo imekuwa ikitunyanyasa tukicheza
nao safari hii tumejiandaa vya kutosha ili tuweze kupata matokeo mazuri
katika mchezo wa nyumbani kabla ya marudiano,”alisema Shime. Serengeti
inahitaji ushindi wa mabao mengi katika mchezo huo kabla ya kurudiana
nchini Congo baada ya wiki mbili na mshindi atafuzu fainali hizo.
0 comments:
Post a Comment