Dar Es Salaam,Tanzania.
MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji anatarajiwa kukabidhiwa rasmi timu
hiyo baada ya mchezo wao wa Ligi Kuu na Simba Oktoba Mosi mwaka huu.
Habari zilizopatikana Dar es Salaam jana zinasema Bodi ya Wadhamini
ya Yanga chini ya Fatuma Karume na Francis Kifukwe imeridhia kumkodisha
rasmi Manji timu hiyo kwa miaka 10 kama alivyoomba kupitia mkutano wa
dharura wa wanachama wa klabu hiyo uliofanyika Juni 11 mwaka huu kwenye
ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam.
Manji aliomba apewe klabu kwa miaka 10 na katika kipindi hicho
atakuwa anachukua asilimia 75 ya mapato ya timu, huku asilimia 25
ikibaki kwa wanachama ambapo pia katika kukodishwa huko timu ya soka na
nembo ya klabu zote zitakuwa chini ya kampuni zake.
“Mkinikodisha ndani ya miaka mitatu nitahakikisha naingiza faida, na
asilimia 25 ya faida itakwenda kwenye klabu, ikiwa ni hasara nitabeba
mimi, na baada ya miaka 10 nitawarudishia klabu yenu muanze kununua
hisa,”alisema Manji katika mkutano huo.
Hivi karibuni Kifukwe alisema kuwa wamesharidhia
kumkabidhi Manji timu na kwamba bado kuna vitu vidogo vidogo
wanakamilisha.“Kimsingi tumeshakubaliana kumkodisha timu, lakini kuna marekebisho
madogo madogo katika ‘Proposal’ (Mapendekezo) yake ni lazima yafanyiwe
marekebisho kabla ya kumpa rasmi,” alisema.
Lakini hata hivyo jana mmoja wa vigogo wa klabu hiyo alithibitisha kuwa Manji atakabidhiwa timu hiyo baada ya mchezo na mahasimu
wao. Hata hivyo, Kifukwe jana alipoulizwa kuhusu kumkabidhi Manji timu
baada ya Oktoba Mosi alisema “Kwa upande wetu tumeshamaliza, suala hilo
kwa sasa lipo mikononi mwa Kamati ya Utendaji ya Yanga, wao ndio
wanapaswa kuzungumzia suala hilo”.
Kwa upande wa Katibu wa Yanga, Baraka Deusdetit alipoulizwa kuhusiana
na suala hilo alisema: “Hilo suala ni la Bodi ya Wadhamini vipi lirudi
kwenye Kamati ya Utendaji, nadhani bodi ya wadhamini ndio wanapaswa
kuzungumzia suala hilo, inawezekana mchakato bado haujakamilika ndio
maana wanasita kuuzungumzia, ukikamilika utawekwa wazi hakuna cha
kuficha,” alisema.
0 comments:
Post a Comment