Alexandria,Misri.
MIAMBA wa Misri Zamalek wamejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika baada ya Ijumaa usiku kuibuka na ushindi mnene wa mabao 4-0 dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco katika mchezo wa kwanza wa hatua ya nusu fainali uliochezwa katika uwanja wa Borg El-Arab huko Alexandria.
Iliwachukua Zamalek dakika 4 tu kuandika bao la kuongoza lililofungwa na Mahmoud Abdel Razek Fadlallah maarufu kama Shikabala kwa mkwaju mkali wa mita 30.
Bao la pili limefungwa na Aymen Hefny katika dakika ya 18 baada ya kuwazidi ujanja walinzi wa Wydad Casablanca na kufanya Zamalek iende mapumziko ikiwa mbele kwa mabao hayo mawili kwa nunge.
Zamalek ilijipatia bao la tatu kupitia kwa Bassem Morsi katika dakika ya 48 aliyefungwa kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Shikabala
Katika dakika ya 65 kocha wa muda wa Zamalek Moemen Soliman alifanya mabadiliko kwa kumtoa mfungaji wa bao la pili Aymen Hefny na kumuingiza Mostafa Fathi.
Mabadiliko hayo yaliinufaisha zaidi kwani katika dakika ya 72 Fathi aliifungia Zamalek bao la nne kwa mkwaju wa penati uliopatikana baada ya yeye mwenyewe kuangushwa ndani ya eneo la boksi.
Timu hizo zitarudiana tena Jumamosi Septemba 24 katika mchezo wa pili wa nusu fainali utakaochezwa katika uwanja wa Stade de FUS huko Rabat,Morocco.
0 comments:
Post a Comment