Dar Es Salaam,Tanzania.
BAADA ya kumaliza msimu uliopita katika nafasi ya nne,kipa wa Azam FC, Aishi Manula,amesema kuwa anaweza kuihama klabu hiyo kama taratibu za uhamisho wake zitafanyika katika njia sahihi.
Manula ndiye Kipa Bora ambaye amechukua tuzo hiyo katika misimu miwili mfululizo.
Hata hivyo Manula ameweka wazi kuwa atafurahi zaidi akipata klabu ya nje ya nchi ambayo anaamini itasaidia kuboresha kiwango chake na kuisaidia timu ya Taifa (Taifa Stars).
Akizungumzia hili,Manula, alisema kuwa bado ana mkataba na klabu yake lakini hilo linaweza kuzungumzika endapo timu inayomtaka itakaa meza moja na Azam FC kufanya mazungumzo.
Manula alisema kuwa anaamini msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakuwa mgumu zaidi kutokana na klabu zote kujipanga kurekebisha makosa yaliyotokea msimu uliomalizika.
"Tutarajie kuwa na msimu ujao mgumu zaidi,kila timu inajipanga na inasajili kikosi imara kwa lengo la kuonyesha ushindani," alisema Manula.
Kipa huyo aliongeza kwa kuwataka waamuzi wanaochezesha mechi za ligi kuchezesha kwa haki na hii itazisaidia timu zinazowasilisha nchi katika mashindano ya kimataifa kufika mbali.
0 comments:
Post a Comment