Kumasi,Ghana.
WAKATI dunia ikiwa bado hataijasahau ajali mbaya ya ndege iliyoua wachezaji 19 wa timu ya Chapecoense ya nchini Brazil pamoja na benchi lao lote la ufundi mwezi Disemba mwaka jana,dunia inapaswa kujiandaa kwa msiba mwingine mkubwa utakaoukumba umma wa wapenzi wa soka hapo mwezi Septemba mwaka huu.
Hii ni kwa mujibu wa Mchungaji mmoja wa nchini Ghana anayefahamika kwa jina la Nabii Reindolph Oduro Gyebi wa kanisa la God’s Crown Chapel lililoko kwenye mji mashuhuri wa Kumasi.
Gyebi ametabiri kuwa mwezi Septemba mwaka huu timu ya taifa ya Ghana,Black Stars itapata ajali mbaya ya ndege na wachezaji wake wote watapoteza uhai pamoja na watu wote watakaokuwa wameambatana na kikosi hicho.
Nabii huyo anayekwenda pia kwa jina la utani la Eagle Prophet,ameongeza kuwa kocha wa Ghana,Kwesi Appiah pamoja na maafisa wa chama cha soka cha nchi hiyo wanapaswa kuonana nae haraka ili kuangalia namna ya kuepusha maafa hayo.
Mchungaji huyo ameyasema hayo jana Jumatano wakati akihubiri kupitia kituo cha redio cha Abusua FM na kusisitiza kuwa amefunuliwa jambo hilo na Mungu wakati akiwa katika maombi yake ya kila siku.
Mbali ya kuitabiria mabaya timu ya taifa ya Ghana,Mchungaji huyo pia ametabiri kuwa gwiji wa soka wa zamani wa nchini hiyo Abedi Pele ambaye ni baba mzazi wa nyota Jordan Ayew na Andre Ayew nae atafariki mwaka huu kwa ugonjwa wa ajabu.
Hii ni mara ya pili kwa mchungaji huyo kuitabiria mabaya Ghana.Mara ya kwanza alitabiri kuwa kungetokea maafa kwenye maporomoko ya Mto Kintampo na utabiri huo ukawa kweli baada ya watu zaidi ya 18 kupoteza maisha katika mto huo kwa kuangukiwa na miti pamoja na mawe walipokuwa wanaogelea.
Ikumbukwe mwezi Septemba mwaka huu timu ya taifa ya Ghana itasafiri kwenda Brazaville kuvaana na Congo katika mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza michuano ya kombe la dunia la mwaka 2018.
0 comments:
Post a Comment