Nice,Ufaransa.
MARIO Balotelli amekianza vyema kibarua cha kuitumikia timu yake mpya ya OGC Nice baada ya Jumapili usiku kuifungia timu hiyo mabao mawili na kuiwezesha kushinda mabao 3-2 dhidi ya Marseille katika mchezo mkali wa ligi daraja la kwanza nchini Ufaransa uliochezwa katika uwanja wa Allianz Riviera huko Nice.
Balotelli alianza kuifungia Nice bao la kuongoza dakika ya 7 ya mchezo kwa mkwaju wa penati uliopatikana baada ya yeye mwenyewe kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari.
Marseille walijibu mapigo baada ya kupata bao la kusawazisha dakika ya 26 mfungaji akiwa Florian Thauvin na kufanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa sare ya kufungana bao 1-1.
Kipindi cha pili Marseille walikianza vyema kwani dakika ya 72 walifanikiwa kuchukua tena usukani wa mchezo baada Bafetimbi Gomis kufunga bao la pili kwa penati.Bao hilo halikudumu sana kwani katika dakika ya 78 Balotelli aliirejesha OGC Nice mchezoni baada ya kuifungia bao la pili kwa kichwa ambalo lilifuatiwa na bao la tatu na la ushindi lililofungwa na Wylan Cyprien dakika ya 87 kwa mkwaju mkali wa mbali.
Ushindi huo umeipeleka OGC Nice mpaka nafasi ya pili ya msimamo ya ligi ya Ufaransa nyuma ya vinara Monaco kwa tofauti ya mabao.Zote zina alama 10 kila moja.
0 comments:
Post a Comment