Uyo,Nigeria.
TIMU ya taifa ya soka ya wanaume ya Tanzania maarufu kama Taifa Stars imewasili salama nchini Nigeria tayari kwa mchezo wake wa mwisho wa kundi G la michuano ya AFCON dhidi ya wenyeji wao Super Eagles.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari kutoka nchini Nigeria vinasema Taifa Stars iliwasili jijini Abuja kwa ndege ya Ethiopian Airline na kupokelewa na Mkuu wa Protocol wa Chama cha soka cha nchi hiyo NFF,Tunde Aderibigbe.
Baada ya mapumziko ya muda mfupi ilisafiri kuelekea Uyo ambako ndiko mchezo utakapochezwa kwa kutumia usafiri wa shirika la ndege la Dana Air na kupokelewa na Katibu Mkuu Msaidizi wa NFF,Dr. Emmanuel Ikpeme na imefikia katika hoteli ya Ibom Le Meridien.
Stars na Nigeria zinatarajiwa kushuka dimbani Akwa Ibom Stadium siku ya Jumamosi katika mchezo ambao utakuwa wa kulinda heshima kutokana na timu zote kushindwa kukata tiketi ya kushiriki michuano ya AFCON.
Mwamuzi wa mchezo huo atakuwa Mehdi Abid Charef kutoka Algeria ambaye atasaidiwa na waamuzi wengine kutoka Algeria,Abdelhak Etchiali,Ahmed Tamen pamoja na Mustapha Ghorbal ambaye atakuwa mwamuzi wa akiba.Kamisaa wa mchezo huo atakuwa Bokinda Inyangi kutoka Congo DR.
0 comments:
Post a Comment