MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania,Mbwana Ally Samatta,ameiokoa klabu yake ya KRC Genk kulala ugenini baada ya kutoa pasi iliyozaa bao la pili na la kusawazisha dhidi ya klabu ya Royal Excel Mouscron katika mchezo ulioisha kwa sare ya mabao 2-2 huko katika dimba la Stade Le Canonnier.
Wenyeji Royal Excel Mouscron ndiyo waliokuwa wa kwanza kuuona wavu wa KRC Genk baada ya Mshambuliaji wa Misri, Trezeguet,kufunga katika dakika ya 2 ya mchezo.Bao hilo lilizimwa katika dakika ya 32 baada ya Nikos Karelis kuisawazishia KRC Genk akitumia vyema pasi ya Alejandro Pozuelo.
Katika dakika ya 42 Royal Excel Mouscron walikamata kwa mara nyingine uongozi wa mchezo huo pale Valentine Viola alipofunga bao la pili akiunganisha krosi safi ya Mmisri,Trezeguet,na kuifanya miamba hiyo iende mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-1.
Kipindi cha pili mabadiliko yaliyofanywa na Kocha wa KRC Genk katika dakika ya 67 ya kumtoa Leon Bailey na kumuingiza Mbwana Samata yalizaa matunda baada ya Nikos Karelis kuifungia KRC Genk bao la pili na la kusawazisha akimalizia pande safi kutoka kwa Samatta na kufanya mchezo uishwe kwa sare ya kufungana mabao 2-2.
0 comments:
Post a Comment