Mohamed Kiganja
Dar Es Salaam,Tanzania.
Kaimu Katibu Mkuu wa BMT,Mohamed Kiganja,amefafanua taratibu zinazotakiwa kufuatwa ili timu ikodishwe.
Kiganja amefafanua kuwa taratibu hizo ni kutumia vikao,ambapo cha kwanza ikiwa ni Kamati ya Utendaji ya Klabu itakayochambua hoja na kukubaliana au kutokukubaliana kisha kupeleka katika kikao cha ngazi za juu.
Pia, amesema baadaye hoja inapelekwa kwenye mkutano mkuu wa wanachama wote uwe wa dharura au kawaida ili kujadiliana hoja husika, kisha baada ya kukubaliana au kutokukubaliana inapelekwa kwa Baraza la wadhamini lenye uwezo wa kuingia kwenye maamuzi makubwa, na mwisho inapelekwa kwa msajili.
“Kwa mujibu wa sheria ya BMT ya mwaka 1967 kifungu namba 11 (1) kinaeleza chama chochote kinachofanya mabadiliko ya jina,anuani, madhumuni au kifungu chochote cha Katiba yake kitatakiwa kipate idhini ya msajili,”alisema.
Alisema kifungu namba 11 (3) msajili anaweza kuyakataa maombi ya kubadili kifungu chochote cha katiba kama ataona kuwa mabadiliko yanaweza kuhatarisha usalama na kuvuruga amani, au kama kuna malengo ya kuwanufaisha wachache au kama hayazingatii sera za michezo na sheria za BMT.
Alisema baada ya hatua hizo kukamilika, inabidi kufanya marekebisho ya Katiba ambayo yatapitia kwenye taratibu za klabu na ndipo klabu husika itakuwa imepata baraka za serikali.
0 comments:
Post a Comment