Dar Es Salaam,Tanzania.
KOCHA Mkuu wa Stand United ya Shinyanga, Patrick Liewig ameutupia
lawama uongozi wa timu hiyo kwa kutoonesha ushirikiano wa kumsaidia kupata kibali cha kuishi na kufanya kazi nchini, baada ya kile cha awali kuisha muda wake.
Mfaransa huyo alisema tangu kujitoa kwa waliokuwa wadhamini wa timu hiyo Kampuni ya Uchimbaji Madini ya ACACIA, mambo yamekuwa yakifanywa bila mpangilio kwenye timu hiyo kiasi hata wachezaji na benchi la ufundi kushindwa kulipwa mishahara na posho zao.
Akifunguka,Liewig,ambaye kwa sasa yupo Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kupata kibali kipya,alisema mambo yote hayo aliwaarifu viongozi wake akiwemo mwenyekiti wa Stand United, Ellyson Maeja ili amsaidie lakini hakufanikisha.
“Nimeamua kujiweka pembeni na timu ili kushughulikia taratibu za kupata kibali cha kuishi hapa nchini,kile cha kwanza kimekwisha na uongozi wa Stand United haujaonesha jitihada za kunisaidia kupata, katika hili kuna mambo mengi yamekuwa yakienda ndivyo sivyo hasa baada ya kujiondoa kwa ACACIA,” alisema Liewig.
Mbali ya hayo ya kumalizika kwa kibali cha kufanyia kazi pia kocha huyo aliyeiwezesha timu hiyo kuanza vizuri msimu huu na kushika nafasi
ya pili kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 16 nyuma ya vinara Simba kabla ya mechi yake ya jana dhidi ya Azam, alisema yapo mambo mengi maovu yanafanyika ndani ya timu ikiwemo hujuma.
Kocha huyo alikwenda mbali zaidi baada ya kumtuhumu msaidizi wake Athuman Bilali ‘Billo’ akipanga kuhujumu timu na baadhi ya wachezaji.
Alisema kocha huyo alikuwa akiwashawishi wachezaji muhimu (anawataja) kufanya hujuma na lengo ni kufanya yeye (Liewig) aonekane si bora na hana uwezo.
“Tatizo hilo la hujuma halipo kwa kocha msaidizi bali hata kwa Mwenyekiti Maeja, ambaye kabla ya mchezo wetu na Yanga aliahidi kuwalipa mishahara wachezaji, lakini zikiwa zimebaki siku mbili kiongozi huyo akaja na kuniambia fedha zile hazipo badala yake niongee na
wachezaji ili kuwapa ari wacheze badala yake watawapa posho kwa kutumia fedha za matangazo ya Azam Tv,” alisema.
Alisema hali kama hiyo ilijitokeza kwenye mchezo wao na Majimaji waliocheza ugenini na kushinda mabao 2-0, lakini alijitahidi kusimama kidete na hatimaye kupata ushindi huo pia jambo hilo lilimtokea Mbeya kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City kwa Maeja na msaidizi wake Bilali,kuwachanganya
wachezaji kwenye mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo lakini alijitahidi kuzungumza nawachezaji na kufanikiwa kupata sare.
Baada ya kuona mambo yanazidi kuwa magumu, kocha huyo anasema alizungumza na Mwanasheria wake
Franck Nicolleau awaambie waajiri wake wavunje mkataba maana hawezi kufanya kazi isiyoendana na weledi.
0 comments:
Post a Comment