Uongozi wa Simba
umesema umeamua kulifikisha polisi sakata la usajili wa kiungo mshambuliaji
Ramadhani Singano 'Messi' ili kulinda taswira ya klabu hiyo.
Messi anadai
kutotambua uhalali wa mkataba wake wa miaka mitatu na Simba uliopo katika
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) huku akisisitiza ana mkataba wa miaka miwili
na klabu hiyo ya Msimbazi utakaomalizika Julai Mosi mwaka huu.
Hajji Manara, msemaji
wa Simba, katika mahojiano na moja ya vituo vya redio jijini hapa leo, amesema
kuwa kutokana na mvutano ulioibuka baina ya pande zote mbili, klabu imeona ni
vyema kulifikisha suala hilo mbele ya vyombo vya dola ili lipatiwe ufumbuzi.
"Simba ni taasisi
kubwa, suala hili linachafua 'image' (taswira) ya taasisi hii. Tukumbuke pia
kwamba Simba ina wadhamini. Inaposdemwa kwamba tumeghushi nyaraka likiwamo dole
gumba la Messi, ni kashfa kubwa. Wadhamini wanatuelewaje?" Amehoji Manara
bila kutaja lini hasa suala hilo litatinga polisi.
Wakati Simba
wakitishia kulifikisha suala hilo mikononi mwa polisi, tayari Chama cha
Wachezaji wa Soka Tanzania (Sputanza) kimeshalifikisha sakata hilo mikononi mwa
TFF ili litatuliwe na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya shirikisho
hilo.
Mwenyekiti wa
Sputanza, Mussa Kisoky, alisema jijini jana kuwa walifikia hatua ya kuonana na
uongozi wa TFF baada ya kupewa maelezo na winga huyo mwenye umri wa miaka 21.
0 comments:
Post a Comment