728x90 AdSpace

  • Latest News

    Tuesday, June 23, 2015

    MAKALA!!MEMPHIS DEPAY, ACHANA NA DIBAJI TUNAYE ASHLEY YOUNG

                                            Tokeo la picha la memphis depay
    Unaponuna siku zote basi nuna kwa sababu,  unapocheka pia fanya kwa sababu na ukiamua fanya vyote kwa sababu maalumu. Ni kama ambavyo kuna namna moja tu ulimwenguni ambayo unaweza kuuchukia usajili wa Memphis Depay, 
    nayo ni kuwa adui ama kutokuipenda Manchester United.

    Utamchukia vipi mchezaji anayeweza kukuonjesha ladha ya magoli 20 akitokea pembeni. Hii ni moja ya baraka zilizoikuta ama zitakazoikuta ligi kuu ya Uingereza pamoja na Manchester United . Kuna kila namna ambayo jicho lako ng'aavu linaweza kunufaika na ujio wa huyu mtu.  Walau kiasi fulani liachane na kadhia ya yule Ashley Young,  Valencia,  wale akina Sterling na wengine wasio na mnyumbuliko na madoido kadha wa kadha . Ukiwa na Depay ambaye ni bora unakuwa umepata muuza sura kama Neymar,  umepata miguu ya kupiga adhabu na mashuti ya mbali kama yule Cristiano Ronaldo mdogo,  unakuwa na mtu anayejisikia na kujua nini maana ya biashara. Mwisho anakukosha kwa picha zake kali mwisho wa msimu alizopiga na Irina Shayk wa Ronaldo kule Ibiza Spain, kitu ambacho ligi kuu ya Uingereza na vyombo vyake vya habari vimekikosa kwa Muda mrefu.
    Kuna wakati nawaza na pia  najiuliza kama kuna usahihi wa yeye kwenda pale Manchester United,  na majibu yote Ndio na Hapana yanakuwa majibu sahihi. Pamoja na kutokuwa katika kiwango bora hakuna siri kuwa Manchester United ni klabu inayofanya usajili kwa kiasi kikubwa kwa sasa. Kwa umri wake Manchester United inaweza isiwe sehemu sahihi sana. Lakini kwa kipaji chake ni mahala stahiki kabisa. Lakini ligi ya Uingereza ni tofauti sana, ina kasi kuliko mchezaji, ina vurugu kuliko mchezaji na pia ina mahitaji makubwa kuliko mchezaji. Ukifika pale kuwa na kipaji ni jambo moja, 

     lakini kukiishi kipaji ndilo jambo la msingi zaidi mahala ambapo inaweza kuwa changamoto kwa mchezaji wa umri wa Depay. Kwa umri wake ni rahisi kutabiri kuwa Depay atahitaji Muda kiasi kuendana na kasi ya ligi ile,  pamoja na kuwa ni mchezaji mwenye nguvu atahitaji Muda kuzizoea ghasia za stoke city, lakini swali ni je Kuna Muda wa kusubiri katika ligi ya Uingereza na hasa klabu yake ya Manchester United?  Kutakuwa na uvumilivu hasa ukifikiria kuna Di Maria,  Mata na akina Young katika upande huo huo wa uwanja?  Tatizo la Depay hapa sio kipaji lakini presha iliyopo mbele yake. Kutupa sababu ya kumuweka Mata na Young katika mbao, kutupa imani kuwa mzigo kwa Rooney na Van Persie wa mechi 18 za ligi umepungua.
    Tokeo la picha la ashley young
     Yupo katika mikono sahihi ya baba yake Van Gaal lakini hayupo katika jamii sahihi ya waingereza. Jamii iliyofikia hatua ya kuamini Sterling na Young ni bora maradufu kuliko Di Maria,  jamii ambayo itakuimba na magazeti yatakuandika vyema ukifanya vizuri mithili ya malaika mwokozi lakini ni jamii hii yenye sura sita, ambayo ukicheza mechi tano bila goli itamuweka Berahino wa West Brom juu yako kwa makusudi.

    Kuna Muda ama wakati unafika katika maisha,  kuona kunakuwa kuamini. Unaamini unachoona sio unachosikia,  unapenda unachotizama sio unachosimuliwa. Ni kama wakati huu. Bahati nzuri wachezaji wengi waliotoka ligi ya Eredivisie (ligi kuu ya Uholanzi) huwa na wakati mzuri. Sijaona magoli mengi miguuni kwa Hazard,  Sijaona mitindo ya nywele kwa Sánchez,  na pia hata yule Di Maria hajawahi kuwa mtu wa matangazo. Lakini Depay aliyetulia anakupa vyote hivi. Hakuna njia yoyote Depay anaweza kuwa bora kama Manchester United ikisuasua msimu ujao,  hakuna njia rahisi kwa Depay kama Di Maria wa Madrid akifunga safari kwenda Manchester United,  Kuna ufinyu kwa Depay kama Mata aliyemaliza msimu akianza pia,  usisahau mahitaji ya Rooney uwanjani na uwezekano wa mshambuliaji mpya. 

    Lakini Depay anabaki kuwa Depay,  miguuni kwake Kunabaki alama za kipekee,  bado naamini kama amefunga safari vyema basi ni baraka njema na neema kwa Manchester United. Malezi yake hayatakuwa na ugumu sana,  kinachotakiwa ni umahiri wake tu. Hata hivyo ndo kwanza maisha ya Depay yapo katika Dibaji,  Yale magoli yake ya Psv na timu ya Taifa ni utangulizi tu,  kitabu bado hajakikamilisha hasa wakati huu ambapo hatopambana na mbinu za Frank DE Boer,  wakati mnawaza nani atamkaba Depay,  wa kwanza ninae kichwani, wala hatoki mbali anaitwa Ashley Young. Unamkumbuka Luis Nani,  Kisha Di Maria. Hata huyu anafuata hiki. Depay anatakiwa aendelee na uandishi wa kitabu chake, Hii Dibaji wanayojivunia nayo mashabiki wa Manchester United tumeshaisoma, akizubaa mwisho wa msimu nitamkumbusha kuwa kila siku jamii ya Waingereza tunaye Ashley Young na sisi ni wanafki kweli na kitabu chake hakitakamilisha walau sura moja.

    Ahsanteni. By Nicasius Coutinho Suso
    Usisahau kunifollow
    Instagram @NicasNicho
    Twitter @NickieNicas
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: MAKALA!!MEMPHIS DEPAY, ACHANA NA DIBAJI TUNAYE ASHLEY YOUNG Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top