Wakati klabu za Yanga na Azam zikiwa kwenye maandalizi ya michuano ya Kombe la Kagame, Simba yenyewe imetulia ikizivutia pumzi kabla ya kuwashtukiza katika Ligi Kuu Bara ijayo.Azam na Yanga zimekuwa zikiibania kuingia katika Mbili Bora
ya Ligi Kuu kwa misimu mitatu mfululizo sasa na kuikosesha ushiriki wa michuano ya kimataifa.
Hata hivyo uongozi wa klabu hiyo kupitia Kamati yake ya Usajili na ile ya Ufundi, imekaa chini na kufanya mambo yake kwa umakini kupitia usajili inayoendelea kuufanya ili wasije wakabugi tena.Kamati ya Usajili chini ya Mwenyekiti wake, Zakaria Hanspoppe, ilianza kwa kuwatema mapro Dan Sserunkuma na Joseph Owino raia wa Kenya na Uganda, kisha ikawavuta fasta Peter Mwalyanzi toka Mbeya City, Mohammed Fakhi wa JKT Ruvu na Mohammed Abdulrahman wa JKU Zanzibar.
Hawakutosheka waliwaongeza Samir Haji Nuhu na Laudit Mavugo wa Vital’O na sasa inadaiwa kumalizana na beki wa Nimuboma Emily wote wakitokea Burundi, ingawa Hanspope alisema siyo kama usajili ndiyo umeishia hapo.
“Nani kakuambia tumemaliza, hatufanyi kwa papara na kutaka kuwafurahisha au kuwaonyesha watu, tunafanya kazi kwa umakini wanaotubeza wakione cha moto msimu ujao,” alisema.Hanspoppe alisema tofauti na watu wanaosema kuwa Simba inasajili kwa nia ya kutetea nafasi ya tatu iliyokamata msimu uliomalizika karibuni, ila ukweli wao wanajipanga kwa ajili ya michuano ya kimataifa wakiamini msimu ujao utakuwa ni wao kwa namna wanavyojipanga.
Juu ya kocha mpya atakayechukua nafasi ya Goran Kopunovic, Hanspoppe alisema Msimbazi wasubiri kwani mazungumzo na kocha wao kutoka Uingereza yamefikia patamu.Kwa miaka mitatu sasa Simba haijashiriki michuano ya kimataifa, wala kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kuzidiwa kete na Yanga na Azam ambazo zimekuwa zikipokezana nafasi ya uwakilishi wa nchi katika Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa Afrika.
0 comments:
Post a Comment