Dar es Salaam. Serikali imesema kuanzia Julai mosi mwaka huu, ajira za utumishi wa umma zitakuwa zikiombwa kwa njia ya mtandao, ili kuongeza ufanisi wa mchakato wa kuwapata watumishi wenye sifa na kupunguza malalamiko ya kupotea kwa barua za maombi.
Akizindua baraza la
kwanza la wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Sektretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani alisema mtandao huo umezinduliwa na waombaji watapaswa kuingia katika tovuti maalumu ya ajira na kutuma maombi yaliyoambatanishwa na vyeti vya taaluma walizosomea.
“Maombi kwa njia ya mtandao yatapunguza kazi ya kuchambua maelfu ya barua za maombi ya kazi zilizokuwa zinatumwa,itapunguza pia manung’uniko kwamba barua zimetumwa kisha zimekaliwa tu,”alisema Kombani.
Waziri huyo, alisema kwa kutumia utaratibu huo mpya, wananchi wanaotaka ajira serikalini watakuwa na uhakika kuwa barua zao zimefika na kupokewa na wahusika. Pia, wanaweza kupata mrejesho kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu zao za mkononi.
Kwa upande wake Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Xavier Daudi alisema baada ya kuona mchakato wa kuajiri unachangamoto nyingi,waliamua kubuni mfumo wa kuomba ajira kupitia mtandaoni.
“Utaratibu huu utatupunguzia gharama,wanafunzi wanaohitimu kila mwaka vyuoni ni maelfu kwa maelfu na nafasi tunazopata serikalini kupitia sekretarieti ya ajira hazizidi 12,000 kila mwaka,” alisema Daudi.
Hata hivyo, katibu huyo alisema wamekuwa wakipata changamoto kubwa kutokana na baadhi ya waombaji kutumia vyeti vya kughushi na hivyo kulazimika kwenda kwenye vyuo husika kuvithibitisha.
0 comments:
Post a Comment