Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia kwa Rais wake Jamal
Malinzi, jana usiku lilitoa ofa kwa wazazi (baba na mama) wa Simon Msuva
kuhudhuria mechi mbili za timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ itakapokuwa ikicheza
dhidi ya Uganda kwenye michezo ya awali kuwania kufuzu kushiriki michuano ya
Afrika inayoshirikisha wachezaji wa ligi za ndani (CHAN).
Malinzi ametoa ofa hiyo kwa wazazi wa Msuva ambaye jana alitangazwa kuwa
mchezaji bora wa ligi kuu ya soka Tanzania bara iliyomalizika Mei 9 mwaka huu
ikiwa kama zawadi na shukrani kwa wazazi hao mara baada ya wazazi wa Msuva
kueleza njia ndefu aliyopita mtoto wao kufikia mafanikio anayoyapata hivisasa
na wao kusimama nyuma yake kwa kila jambo gumu na rahisi alilopitia kijana wao.
Malinzi amesema kuwa, amevutiwa na jinsi wazazi hao walivyosimamia na
kukilea kipaji cha mtoto wao hivyo, TTF imeamua kuwapongeza kwa hatua hiyo na
itagharamia kila kitu ili wazazi wa Msuva wapate kumuona kijana wao akicheza
uwanjani kuiwakilisha Tanzania kwenye mechi dhidi ya Uganda itakayochezwa
Zanzibar Juni 20 na ile ya marudiano itakayopigwa jijini Kampala huku TFF
ikigharamia kila kitu kuanzia usafiri, gharama za viingilio, chakula na malazi
ya wawili hao.
“Nimeguswa sana na maneno ya baba yake Msuva, ameongea maneno mazito sana
ambayo yanaonesha ni jinsi gani amehangaika kutafuta mafanikio ya leo ambayo
kijana wao (Simon Msuva) anayapata. Ni safari ndefu sana wamepitia na
wanahitaji pongezi za dhati na ni mfano wa kuigwa na wazazi wengine”, alisema
Malinzi huku akionekana kuvutiwa na wazazi wa Msuva.
“Kwasababu hiyo, kama TFF tunawaomba mhudhurie kumshuhudia mtoto wenu
atakapokuwa akicheza kwenye timu ya Taifa wakati ikicheza dhidi ya Uganda
mchezo utakaofanyika Zanzibar Juni 20, pia vilevile kwenye mchezo wa marudiano
utakaochezwa jijini Kampala. TFF itagharamia kila kitu kuanzia usafiri,
viingilio, malazi na chakula , karibuni sana kwenye mechi hizo”, alisema
Malinzi.
Awali baba yake Msuva alisema, amepata changamoto nyingi sana wakati
anahangaika huku na kule kuhakikisha mwanae anafanikiwa katika mchezo wa soka
ambao alionesha kuuhusudu tangu akiwa kijana mdogo. Mzee Msuva alisema, ilifika
wakati aligombana na mama yake Msuva kwasababu ya kumtafutia Msuva timu ya
kucheza wakati mama yake alikua anahitaji Msuva aelekeze nguvu zake zote kwenye
elimu akiamini ndiyo itamletea mafanikio maishani.
“Nimehangaika sana na Msuva kabla hajapata mafanikio aliyonayo leo,
ilifikia wakati nagombana na mama yake kwasababu ya mpira. Mama yake Msuva
alikuwa akitaka mtoto aelekeze nguvu zote shule lakini mimi nilikuwa nyuma ya
Msuva kuendeleza kipaji chake cha kucheza mpira alichokionesha tangu akiwa
mdogo. Sikumzuia kwenda shule, ila nilikuwa nahakikisha anapata pia nafasi ya
kucheza mpira”, alisema mzee Msuva.
“Nimezunguka naye kwenye timu nyingi sana nikimpeleka akapate nafasi ya
kucheza kabla hajatua Yanga ambapo wengi wametambua uwezo wake akiwa hapo.
Kwakweli namshukuru sana Mungu kwa mafanikio haya aliyopata kijana wetu lakini
naishukuru pia Yanga na watu wengine wote waliochangia mafanikio haya ya
Msuva”, aliongeza mzee Msuva.
Msuva yupo na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ambayo imepiga kambi nchini
Ethiopia kujiandaa na mchezo dhidi ya Misri utakaopigwa nchini Misri Jumapili
Juni 14 mwaka huu kuwania kufuzu kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika
(AFCON). Jana aliwakilishwa na wazazi wake kwenye hafla ya ugawaji tuzo kwa wachezaji,
timu, makocha na waamuzi waliofanya vizuri kwenye ligi ya msimu wa 2014-2015
iliyomalizika hivi karibuni.
0 comments:
Post a Comment