MAKALA YA LEO
Paul Manjale
Moja kati ya sifa kubwa za mashabiki wa mchezo wa soka duniani ni
kubadilika badilika kama vinyonga. Mashabiki wa soka ndivyo tulivyo
hatutabiriki kama ajari za barabarani,mchezaji tunayempenda sana ndiye
tunayemchukia sana siku tu akifungasha vilivyovyake na kutimka.
Kilichomkuta Okwi jana uwanja wa taifa ni muendelezo tu wa kile ambacho
kimekuwa kikiwakuta nyota wengi wa soka duniani kote.Kuzomewa kila
dakika wawapo uwanjani.Samir Nasri,Robin Van Persie na Emanuel Adebayor
ni baadhi tu ya wachezaji wanaokumbana na kadhia hiyo karibu kila siku
iendayo kwa Mungu.
Okwi akifanya vitu vyake uwanjani juzi dhidi ya Gor Mahia |
Okwi anaingia katika orodha hiyo ya wachezaji wanaozomewa viwanjani
kwasababu tu wametoka upande huu na kuhamia upande ule wa mji tena kwa
watani wa jadi.Yanga kwenda Simba tena katika usajili wenye utata
mkubwa.
Swali la kujiuliza hapa ni kwanini Okwi alizomewa jana kiasi kile na
mashabiki wanaodhaniwa kuwa ni wa klabu ya Yanga?Jibu liko wazi kabisa
ni kwasababu ameiacha Yanga ikiwa mikono mitupu haina taji haina
chochote na yeye kutimkia Simba.
Mashabiki wanamuona Okwi kuwa ni mkosefu na msaliti mkubwa bila hata ya
kutaka kujua nani anaongea ukweli kati yake na viongozi wa klabu
yao.Hakuna tena shabiki wa Yanga anayemuongea Okwi kwa mazuri hata wale
wachache walibahatika kuwa na namba zake za simu siyo ajabu nao wakawa
wameshazifuta mpaka sana.Wanamchukia na kumlani kama mbu wa dengue.
Mashabiki tunasau kuwa soka ni ajira kama zilivyo ajira nyingine hivyo
mchezaji anapohama hapa na kwenda kule ama kule na kuja huku huwa ni
katika kutafuta maslahi mazuri pamoja na mazingira bora kwa ajili ya
soka yake.Ridhiki ya mtu iko miguuni kwake.
Kama tujuavyo ili mchezaji yoyote yule aweze kucheza katika kiwango bora
anahitaji mazingira yatakayompa nafasi ya kufanya hivyo kitu ambacho
Emanuel Okwi anaamini kinapatikana Simba pekee na siyo kwingineko.
Tumemuona jinsi Okwi wa Yanga alivyokuwa mpole kiwanjani kama faru wa
kuchora, hakuwa na makeke wala vurugu zile tulizozizoea kuziona toka
kwake.Hakuwa yule Okwi wa miaka miwili nyuma yule aliyechukiwa na karibu
kila shabiki wa timu pinzani.
Yule Okwi aliyefanya makocha wengi wafanye
kazi ya ziada kuwafunda walinzi wao ili Mganda huyo asilete balaa.
Swali la kujiuliza hapa ni kwanini nyota kama Thierry Henry ana
Christian Ronaldo wanaabudiwa sana Arsenal na Manchester United licha ya
kuwa walivikacha vilabu hivyo kitambo?Jibu ni kwasababu waliifanya kazi
yao barabara,wakashusha mvua ya mataji pale Emirates na Old Trafford na
kisha wakaondoka zao.
Okwi ameondoka na deni Yanga,hakuondoka kama alivyoondoka Henry kwenda
Barcelona ama Ronaldo kwenda Real Madrid.Je,zomea zomea ndiyo dawa ya
kupoza maumivu ya kukimbiwa?sijui tuwaulize hao waliokwenda taifa jana
kumzomea.....Okwi mashabiki ndivyo tulivyo!!
0 comments:
Post a Comment