728x90 AdSpace

  • Latest News

    Monday, September 01, 2014

    KUMBE TATIZO LA MPIRA WA NCHI YETU HALIKUA PESA.

    Richard Leonce Chardboy
    twitter:@chardboy77
    simu:0766399341
    email:chardboy74@gmail.com


    Mungu amenibariki sana kuzaliwa katika kizazi hiki, amenibariki zaidi
    kwa kuniweka Tanzania, nchi yenye kilometa za mraba zaidi ya 945,200.
    Lakini bado ina tatizo la upungufu wa viwanja vya michezo na maeneo ya
    wazi.
    Hapa unaizungumzia nchi inayoshika nafasi ya 31 kwa ukubwa duniani na
    ina watu wanaopenda sana michezo hususani mpira wa miguu.
    Ina mashabiki ambao huwa wanalia machozi pale refa anapotoa kadi
    nyekundu kwa wachezaji wa timu zao. Ina mashabiki ambao pamoja na
    viingilio vikubwa vya mechi, bado wanajitahidi kwenda viwanjani ambako
    pia huambulia maumivu kwa timu zao kufungwa na timu za nje lakini bado
    wanaenda tena katika mechi ijayo.
    Tanzania bado ina mashabiki, hususani wa vilabu vikubwa vya Simba na
    Yanga ambao husafiri na timu hizo kila zinapokwenda kwa ajili ya
    kuzishangilia.

    Najivunia sana kuwa raia wa hii nchi kwa kweli.
    Najivuna kwa sababu nimeshuhudia kipaji murua cha Edibily Jonas
    Lunyamila. Kuna beki wa zamani wa Sports Club Villa ya Uganda, soka
    yake ulitamatishwa na chenga ya Lunyamila mwishoni mwa miaka ya 1990.
    Nikashuhudia ulinzi wa Boniface Pawasa, beki maridadi sana kuwahi
    kumshuhudia akiichezea Simba ya Dar es Salaam. Pawasa alikua vizuri
    sana. Kuna kipindi Simba waliweka kambi kwenye hoteli ya Bahari Beach,
    basi Pawasa alikuwa anakimbia kutoka Bahari Beach mpaka uwanja wa
    uhuru akiwaacha wenzake wanasubiri basi kwenda mazoezini.
    Nikamuona Mohamed Banka akicheza kwa madaha, nikamwona Abdallah Juma
    Akifunga kadiri ya mapenzi yake.
    Nimeona mengi lakini mwisho nikaona mikono ya dhahabu ya Juma Kaseja.
    Namheshimu sana Juma na ninamwandika leo si kwa sababu ya uwezo wake
    tu, bali kwa hiki kitu cha ajabu ambacho wengi tulidhani ni tatizo la
    soka letu.
    Pesa.
    Wakati Juma Kaseja anaichezea timu ya taifa ya Tanzania kwa mara ya
    kwanza, posho waliyokuwa wakilipwa wachezaji kwa siku ilikuwa shilingi
    1500/- kwa siku. Hiyo siyo zamani sana, ni miaka hii hii ya 2000.
    Timu haikuwa siyo tu na jezi za mazoezi, bali hata jezi maalumu ya
    timu ya Taifa ilikuwa haijulikani. Kama unaijua jezi ya Timu ya Taifa
    kabla ya mwaka 2006 hebu nisahihishe.
    Tulikuwa na vifaa duni, uwanja wa mazoezi wa Karume mbovu, timu
    inasafiri kwa basi tena masafa marefu tu, wachezaji wanafanya mazoezi
    na jezi za vilabu vyao na mambo mengine mengi tu ya kusikitisha sana.
    Kwa wakati huo tuliamini tatizo ni pesa, tuliota kwamba siku tukipata
    pesa, tutafanya vizuri tu.
    Tuliamini hivyo kwa sababu hatukuwa na pesa. Tulitamani angalau
    kuwalipa wachezaji wetu posho ya shilingi hata 10000/- kwa siku lakini
    hatukuwa nazo.
    Kilia mtu aliamini tulifanya vibaya kwa sababu hatukuwa na pesa na
    tungefanya vizuri kama tungepata pesa. Hivi ndivyo akili ya masikini
    yeyote ilivyo. Kijana masikini anaamini akipata pesa ataoa mwanamke
    mzuri na atakuwa na furaha.
    Miaka ikaenda, Juma Kaseja na wenzake akina Tomas Mashala, Alphonce
    Modest na Mecky Maxime wakaendelea kuitumikia nchi yetu tu hivyo
    hivyo, wakifungwa tunawatukana, wakishinda tunaamini wangeweza zaidi
    kama tungekuwa na pesa.
    Kizazi chao kikapungua, Juma akaja kucheza tena na kizazi cha akina
    Henry Joseph, Nizar Khalfan na Amir Maftah.
    Hawa walipata pesa, walipata pesa ambayo Juma hakuwahi kutarajia
    kwamba anaweza kuipata akiwa na timu ya Taifa.
    Tukaamini kwamba tutafanya vizuri kwa sababu tumeanza kupata wadhamini
    na wanawapa wachezaji wetu pesa.
    Tukaanza kutengeneza yimu ya vijana, akina Jery Tegete, Yusuph Mgwao,
    Kiggi Makasy na Mrisho Ngassa. Tukasema hii ikikua itatupa furaha kwa
    sababu sasa tuna pesa.
    Lakini ikawa kinyume. Wakacheza mpaka sasa wanaitwa wakongwe, bado
    hawakutupa ambacho tulikitarajia.
    Tukajiuliza tatizo ni nini? Labda tatizo ni kocha. Tukamwondoa kocha
    wetu kipenzi lakini hatukufanikiwa kufanya vizuri.
    Ninapoandika makala haya kwa uchungu sana, wachezaji wa Timu ya taifa
    wapo kambini. Huko wanalipwa posho ya shilingi 50,000 kwa siku ambayo
    siyo ndogo kwa sababu maisha ya Mtanzania wa kawaida tunayajua.
    Timu inakaa katika kambi nzuri, ina vifaa mpaka vya ziada. Tuna pesa
    nyingi lakini bado nyavu za wapinzani hazichezi. Labda moto umepishana
    na dhahabu na sasa dhahabu haing'ai. Labda sasa tuna pesa ila hatuna
    tena wachezaji wazuri na ndio maana TFF waliamua kutumia pesa kutafuta
    vipaji nchi nzima. Kazi ambayo haiwahusu kwa sababu timu ya Taifa siyo
    klabu.
    Pamoja na kuwa na pesa sasa hivi, bado timu yetu ya taifa haieleweki
    inavaa jezi gani, inabadili jezi kulingana na upepo wa maisha.
    Hatusemi watumie jezi ile ile na isiboreshwe, hapana. Lakini basi kwa
    nini hatuna rangi maalum ya timu ya Taifa ambayo hata mashabiki
    wanavaa?
    Kwa sababu tuna pesa nyingi leo, tukataka tutumie baadhi yake kufanya
    mchakato wa kubadili jina la timu ya Taifa. Sijui hili lililopo lina
    tatizo gani, shukrani za dhati kwa serikali kwa kusitisha mpango huo.
    Pesa siyo mbaya, na huwezi kuendesha mpira kama huna pesa, lakini
    Sababu ya mchezaji kucheza chini ya kiwango leo hii ni ipi?
    Kuna timu huwapeleka wachezaji wake Uturuki kuweka kambi, inawalipa
    mishahara mizuri kwa wakati halafu wakirudi bado hawafanyi vizuri.
    Kuna timu ina kila kitu, ina uwanja mzuri, ina vifaa, ina mabasi ya
    kisasa, ina timu ya vijana lakini bado haifanyi vizuri kimataifa.
    Kuna timu illijaribu kurudi katika msingi, ikapandisha timu yake ya
    vijana ambayo ilikuwa nzuri. Tukasema ikiaminiwa na ikilipwa vizuri
    itafanya vizuri lakini bado ilipopandishwa haikuleta nzjibu
    yaliyotarajiwa.
    Ndugu zangu, nikiyafikiria yote hayo naanza kuamini kwamba tatizo la
    mpira wetu siyo pesa.
    Tena yawezekana pesa ndiyo mchawi wa soka letu.
    Ndiyo, ni pesa inayotufanya tushindane kumsajili Emmanuel Okwi bila
    kujali kama ataisaidia timu au la.
    Wakati akina Juma wanacheza bila pesa nyingi, ndoto ilikua ni kupata
    pesa siku moja. Na kwa sababu hapa kwetu pesa ndio kila kitu basi
    baada ya pesa kupatikana tukawa ndio tumemaliza kila kitu pia.
    Bahati mbaya hatuna mwanasoka aliyecheza Ulaya kisha akaja kuimiliki
    Sinza nzima kama wanavyofanya akina Yaya Toure huko Ivory Coast.
    Tungekuwa naye angalau angewaonesha wachezaji wetu kwamba kuna pesa
    nyingi zaidi ya hizi za Azam, Simba na Yanga.
    Tunajua kwamba wachezaji wetu hawana msingi mzuri tangu utotoni,
    lakini mimi naamini kwamba wangeweza angalau kuwa kichwa cha mbwa kama
    wameshindwa hata kuwa mkia wa Simba.
    Hakuna siasa inayompeleka mchezaji Ulaya. Ni kujituma kwake tu. Demba
    Ba alijipeleka Ulaya mwenyewe, hakupelekwa na mtu wanaemsubiri
    wachezaji wetu jamani.
    Namhurumia sana shabiki, shabiki anaumia sana zaidi ya mchezaji pale
    timu inapofungwa kwa sababu yeye hapati chochote, sana sana anaumia
    kwenye daladala, anaumia kwenye kiingilio, anaumia akiporwa pesa zake
    pale uwanja wa taifa. Anatarajia kupona uchungu wake kwa kuona tu
    nyavu zikicheza, tofauti na nyinyi wachezaji.
    Nyinyi mna tabu gani, mkijeruhiwa mnatibiwa, mpira mmepewa vipaji na
    Mungu, mkifungwa mnajipoza na posho. Basi jitumeni, fanyeni mazoezi na
    mfanye vizuri kwenye mechi ili pesa ionekane ndio ilikua tatizo enzi
    za akina Juma.
    Inatia hasira sana, akija kocha anayetoa mazoezi magumu kwa wachezaji
    basi kocha huyo hawezi kudumu katika klabu. Wachezaji wetu wanajua cha
    kufanya ili kocha afukuzwe kwa sababu hapa kwetu kocha sie
    anayewasajili na siye anayewapa mikataba.
    Sijui tatizo ni nini, kwa nini tunapenda sana mpira lakini mpira hautupendi?
    Kama tatizo letu siyo pesa, tatizo letu ni nini?


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: KUMBE TATIZO LA MPIRA WA NCHI YETU HALIKUA PESA. Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top