728x90 AdSpace

  • Latest News

    Wednesday, July 01, 2015

    MASHABIKI WAMPAGAWISHA NGOMA

    Dar es Salaam. Mshambuliaji mpya wa Yanga, Donald Ngoma jana alianza mazoezi rasmi na klabu hiyo na kuwa kivutio kwa mamia ya mashabiki waliofika kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.
    Ngoma na Mghana
    Joseph Tetteh Zutah walisaini mkataba wa miaka miwili kila mmoja mbele ya katibu mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha na mjumbe wa kamati ya usajili wa klabu hiyo, Isaac Chanji.
    Tiboroha alisema uwezo wa Ngoma ambaye alikuwa anachezea FC Platinum ya Zimbabwe unafahamika na Zutah aliyekuwa anachezea Medeama ya Ghana ni ‘mkali’ kutokana na tathmini ya kocha.
    “Tumekamilisha usajili wa wachezaji wa kigeni na sasa tunangalia zaidi maandalizi ya timu, japo tuna mipango ya kuwatoa wachezaji kwa mkopo, bado tunatafakari ni wachezaji gani wa kutolewa kwa mkopo ili kuweza kufanikisha zoezi hilo,” alisema Tiboroha.
    Baada ya mazoezi ya asubuhi kundi kubwa la mashabiki lilimzunguka Ngoma kumpongeza, kisha kumbeba juu kwa juu hadi kwenye gari na kulisukuma, huku Mzimbabwe huyo akishangazwa na hali hiyo ambayo ameeleza kuwa hajawahi kuiona.
    Hata hivyo, mshambuliaji huyo alieleza kufurahia mazoezi hayo na kusema kuwa mbinu za kocha Hans van Pluijm zitamsaidia kuwa kwenye nafasi sahihi na muda sahihi.
    “Nimefurahia kuanza mazoezi leo, nifurahi kuwa hapa, nimeshangazwa na jinsi mashabiki wa Tanzania walivyonipokea tangu siku ya kwanza Uwanja wa Taifa na hata hapa mazoezini, nina furaha, sijui nielezeje kwani sijazoea haya mambo kwetu, maana Zimbabwe, mashabiki wanakusapoti siku ya mechi na huwezi kuwaona wamejaa hivi mazoezini na kukufurahia.
    “Nimefurahi, kwani kocha alivyonipokea, amekaa nami kunieleza mambo ya msingi kuhusu timu na mimi kama mchezaji nijiweke vipi nje na ndani ya uwanja kwa sababu Yanga ni timu kubwa,” alisema Ngoma.
    Aliongeza: “Nimefanya mazoezi kwa siku moja, lakini mbinu za kocha ni nzuri, anaonyesha ana vitu vingi vya kiufundi ambavyo vinaijenga timu na mchezaji kwa jumla, kwani amekuwa akitupa mbinu nzuri na zinamsaidia mchezaji kuwepo kwenye nafasi sahihi na muda sahihi.”
    Katika mazoezi hayo, Ngoma alionekana kukonga nyoyo za mashabiki, hasa uwezo wake wa kumiliki mpira bila kumpa nafasi adui auchukue mguuni mwake na mashuti yake makali aliyokuwa akipiga mara kwa mara na kuamsha kelele kwa mashabiki waliohudhuria mazoezi hayo.
    Beki wa kulia wa klabu hiyo, Zutah naye alionekana na kipaji cha mpira baada ya kuonyesha uwezo wa kutoa pasi, ingawa alionyesha kutokuwa na nguvu ikilinganishwa na Juma Abdul anayecheza nafasi hiyo, ingawa yeye (Zutah) anatumia zaidi akili.
    Kuhusu mikataba ya kuitumikia klabu hiyo, Dk Tiboroha alisema kuwa wachezaji hao wamesaini mikataba hiyo baada ya kufuzu vipimo vya afya pamoja na kuridhishwa na uchezaji wao kupitia kocha Pluijm.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: MASHABIKI WAMPAGAWISHA NGOMA Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top