SAA chache baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kukipiga Yanga akitoka Mgambo JKT, kiungo mshambuliaji Malimi Busungu amefichua kilichomfanya asaini fomu za Jangwani.
Mchezaji huyo aliyefunga msimu uliomalizika hivi karibuni akiwa na mabao tisa akiwa mmoja wa wafungaji bora, kabla ya kusaini mkataba huo wa Yanga, alikuwa akitajwa kuwindwa na Simba.
Hakuna aliyekuwa akitarajia kama
mchezaji huyo angemwaga wino Jangwani wakati ilikuwa ikielezwa kuwa viongozi wa Simba walikuwa wakizunguka naye kwenye magari ili kumshawishi ajiunge na timu yao.
Akizungumza muda mchache baada ya kusaini Yanga,Busungu alifichua siri ambayo hakuna aliyekuwa akiijua dhidi yake.Busungu alisema sakata la winga teleza wa Simba, Ramadhani Singano ‘Messi’ dhidi ya viongozi wake, ndilo lililomfanya aamue kuitosa Simba.
“Unajua mimi ni kijana mdogo,pia soka ndiyo maisha yangu, hivyo nilipokuwa nasikiliza mzozo wa Messi na viongozi wa Simba, nikabaini kuwa Msimbazi kuna ubabaishaji mkubwa,” alisema.
“Hata wakati nikifanya mzungumzo na viongozi wa klabu hiyo, nilibaini wengi ni wajanja wajanja na kuhisi linalolalamikiwa na Messi ndiyo utaratibu wa klabu hiyo na kuamua kuwatosa,” alisema.
Busungu alisema anaamini kutua kwake Yanga kutakuwa msaada mkubwa katika mustakabali wa maisha yake ya soka,hasa akitambua kuwa ni klabu itakayoshiriki michuano ya kimataifa mwakani (Ligi ya Mabingwa Afrika),hivyo kuwa na nafasi ya kujitangaza katika anga hizo.
“Michuano ya CAF na umakini wa viongozi wa Yanga hata wakati nazungumza nao, ni uthibitisho kuwa inaongozwa na watu makini na wenye malengo, tofauti na Simba, ingawa siwezi kuibeza,” alisema.
0 comments:
Post a Comment