728x90 AdSpace

  • Latest News

    Thursday, July 09, 2015

    WABONGO NA UZALENDO WA SOKA LAO


    I

    Moja katika ya vitu ambavyo tunaambiwa vinakosekana kwa Mtanzania wa leo basi ni uzalendo. Hili ni swala ambalo limekuwa likipigiwa kelele katika kila nyanja. Watu hasa wazee wa zamani wanauliza mbona vijana wa leo hamna uzalendo na nchi yenu? Leo hii kila mtu anapenda kitu cha ulaya na Amerika tu. Hakuna tena mtu anayependa tena vitu vya hapa nyumbani.

    Naambiwa miaka ya nyuma mchezaji ulikuwa huwezi kuichezea Simba au Yanga mpaka uchunguzwe na kujulikana kweli wewe si mamluki. Leo hii hakuna tena swala la kuchunguzana. Miaka ya leo Juma Kaseja anacheza Simba anaenda Yanga alafu anarudi Simba na bado anaenda tena Yanga.

    Hakuna swala la uzalendo hapa, kinachoangaliwa ni fedha tu. Kitu ninachotaka kukiangalia hapa si uzalendo wa mchezaji mmoja uwanjani. Nishaandika sana kuhusu swala la wachezaji kutotakiwa kuwa na mapenzi na timu Fulani, kwani si kazi yao kuzipenda timu. Kwanza kwa soka la sasa hivi unategemea kweli Countinho wa Yanga apate donge nono la kwenda Azam akatae kisa ana mapenzi na Yanga? Mbrazil mapenzi na Yanga kayatoa wapi? Si amefuata maisha tu?

    Hapa najaribu kuangalia mapenzi ya sisi mashabiki wa soka. Nimebahatika kutembea sehemu mbali mbali za Tanzania. Kila mahali ninakopita kila mtu ni shabiki wa Manchester United, Arsenal, Chelsea, Real Madrid, Barcelona na nyinginezo. Ukienda Babati hakuna tena shabiki wa Babati Shooting Star, ukienda Lindi hakuna tena shabiki wa Kariakoo, ukienda Moshi hakuna tena shabiki wa Ushirika (sidhani hata kama ipo). Kila mtu sasa hivi ni shabiki wa timu za Ulaya. 

    Hakuna tena zile za wakati ule ambapo unakuta makundi ya mashabiki wamekusanyika kwenye viwanja vya mitaani wakiangalia mechi za kombe la diwani, kombe la mbuzi au kombe la ng’ombe. Kila mtu sasa yuko kwenye runinga anaangalia ligi za nje ya nchi.

    Sikatai hii imeletwa na utandawazi kwani miaka ya nyuma kulikuwa hakuna DSTV au vituo vilivyokuwa vinaonyesha mechi za ligi za nje. Nakumbuka nilianza kuangalia mechi za ligi ya Uingereza msimu wa mwaka 1995/1996 kupitia KBC, lakini hii haikunizuia kuwa nahudhuria kungalia mechi za timu ya mtaani kwetu Machava iliyoko manispaa ya Moshi. Sasa hivi wachezaji wengi wanapoanza kucheza soka la Tanzania ndoto zao kubwa huwa ni kucheza soka katika vilabu vya Simba na Yanga (labda na Azam kwa sasa). Mchezaji wa timu ya Toto Afrika, timu ambayo iko mtaani kwao alipokulia hafikirii kuipandisha timu daraja na kwenda kushinda ubingwa wa Tanzania.

     Anafikiria Simba na Yanga wamuone wamsajili. Na ndio maana sitegemei mchezaji kama huyo anaweza kuwa na mapenzi na timu hizo. 
    Bado naamini hata mchezaji wa soka kushinda kombe na timu ya mtaani kwako ulikokulia kunaleta raha na hisia sana kuliko kushinda na timu ya Simba au Yanga.

    Nakumbuka wakati huo miaka ya 1990’s timu ya Machava kushinda kombe la mbuzi tu ilikuwa ni shamrashamra kama vile tumechukua ubingwa wa Tanzania. Leo hii hakuna tena kitu kama hicho mashabiki wanajichagulia timu Ulaya na wanahamishia huko unazi wao. Shabiki wa leo yuko tayari kulipa maelfu ya shilingi apate kuangalia mpira super sport kuliko kwenda uwanjani kuangalia mechi ya Mbeya City na Prisons, na mchezaji naye hivyo hivyo.  
    Viongozi nao wamekuwa wanachangia sana kuziporomosha hizi timu za mitaani na hivyo kupunguza morali wa mashabiki.

    Mashabiki wengi bado wanaweza kurudi na kuzipenda timu zao iwapo tu zitaanza kuwa na muelekeo chanya. Leo hii Mbeya City ni moja ya timu ambazo naweza nikasema ni mfano wa kuigwa, imeamsha tena hari ya watu kuzipenda timu za mikoa yao kama zamani. Kwani hata kwa timu za Ulaya nyingi zinapofanya vizuri ndio zinapata mashabiki huku Tanzania.

     Leo hii Tanzania kuna mashabiki wa Athletico Madrid (ni baada ya kuchukua ubingwa wa Hispania na kufika fainali ya kombe la Ulaya)
    Kwa waliokuwa wanafuatilia ligi ya Tanzania nadhani wote mtakumbuka changamoto ya timu kama Tukuyu Star na MECCO za Mbeya, Maji Maji ya Songea, Pamba na Toto Africa ya Mwanza, Pilsner, Nyota Nyekundu na Pan Afrika za Dar es Salaam, African Sports na Coastal Union za Tanga, na nyinginezo nyingi. Miaka ya nyuma kidogo niliamini mpenzi wa kweli wa timu ni shabiki na wala si mchezaji ila miaka inaenda naanza kuona hata mashabiki si wa kweli kwenye timu zao.Wanayumba kutokana na mafanikio ya timu uwanjani. 

    By Wilbafos Julius 
    July 9, 2015
    Dar es Salaam, Tanzania
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: WABONGO NA UZALENDO WA SOKA LAO Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top