Timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) inatarajiwa kucheza michezo miwili ya kirafiki na timu ya Taifa ya Misri Vijana wenye umri chini ya miaka 17 (The Pharaohs) jijini Dar es salaam.
Mchezo wa kwanza kati ya Serengeti Boys dhidi ya The Pharaohs utachezwa siku ya Jumamosi, Aprili 2 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, huku mchezo wa pili ukichezwa Jumanne Aprili 5 katika uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Msafara wa The Pharaohs unatarajiwa kuwasili Alhamis tarehe 31, Machi ukiwa na watu 33, wakiwemo wachezaji 25 pamoja na viongozi 8, na wataondoka nchini tarehe 6 Aprili kurudi kwao nchini Misri.
Kikosi cha Serengeti Boys kinachonolewa na makocha Bakari Shime na Sebastian Mkomwa wakishauriwa na Jan Poulsen, kimeendelea na mazoezi katika uwanja wa Karume, zilipo ofisi za Makao za Makuu ya TFF.
Serengeti Boys ilingia kambini takribani wiki mbili zilizopita katika hosteli za TFF zilizopo Karume, kujiandaa na michezo hiyo miwili ya kirafiki ya kujipima nguvu kujiandaa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitakazofanyika mwaka 2017 nchini Madagascar.
Tanzania itaanza kuwania kufuzu kwa fainali hizo mwishoni mwa mwezi Juni, kwa kucheza dhidi ya timu ya Taifa ya Vijana ya Shelisheli.
0 comments:
Post a Comment