Na Paul Manjale.
Recife,Brazil.
Brazil imelazimishwa sare ya mabao 2-2 nyumbani na Uruguayi katika mchezo mkali wa kuwania tiketi ya kufuzu michuano ya kombe la dunia kwa ukanda wa Amerika Kusini.
Brazil ikicheza nyumbani huko Recife usiku wa kuamkia leo ilipata bao la kuongoza kupitia kwa winga Douglas Costa aliyemalizia pasi ya Willian ayewazidi ujanja walinzi kadhaa wa Uruguayi na kutoa pasi kwa mfungaji.
Kuingia kwa bao hilo kuliwaamsha wageni Uruguayi ambao walikuja juu na kufanikiwa kusawazisha kupitia kwa Edinson Cavani.Kazi nzuri ya Neymar iliipatia bao la pili Brazil baada ya pasi yake kumkuta Renato Augusto ambaye alifunga na kuwapa uongozi wenyeji.
Uruguayi tena ilifanikiwa kujitutumua na kufanikiwa kusawazisha kupitia kwa Luis Suarez aliyekuwa akicheza mchezo wake wa kwanza baada ya kumaliza kifungo cha kukosa michezo tisa kwa kosa la kumng'ata mlinzi wa Italia Giorgio Chiellini katika fainali za kombe la dunia la mwaka 2014 huko Brazil.
Kwa matokeo hayo Uruguayi imefikisha pointi 10 baada ya kushuka dimbani mara tano hivyo iko nafasi ya 2,Brazil iko nafasi ya 3 na pointi zake 8 nafasi ya nne inashikwa kwa pamoja na timu za Paraguay na Argentina.
0 comments:
Post a Comment