Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetoa adhabu kwa watu tisa wakiwemo
viongozi, wachezaji na kocha mmoja kwa kupatikana na hatia ya makosa ya
kinidhamu.
Katika kikao chake kilichofanyika juzi (Februari 3
mwaka huu) jijini Dar es Salaam, Kamati hiyo imewafungia mwaka mmoja
viongozi wawili wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA)
Mkoa wa Mwanza kwa kuwashawishi wachezaji wa Mwanza
Queens kugomea
uamuzi halali.
Sophia Tigalyoma (Mwenyekiti) na Katibu wake Hawa
Bajanguo walitiwa hatiani kwa kuwashawishi wachezaji kugomea uamuzi wa
Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya TFF kutupa rufani yao dhidi ya
Kigoma.
Kocha wa Polisi Tabora, Eliakim Christopher amefungiwa
mechi kumi na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa mujibu wa Kanuni ya 39(2)
ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) baada ya kutiwa hatiani kwa kumtukana
refa wakati wa mechi kati ya timu yake na Panone FC iliyochezwa mjini
Moshi.
Wachezaji wa JKT Oljoro FC, Dihe Makonga, Swaleh Idd
Hussein, Ramadhan Mnyambegu na nahodha Shaibu Nayopa wamefungiwa mechi
tatu na faini ya sh. 300,000 kila mmoja kwa kuzingatia kanuni ya 36(10)
ya FDL kutokana na kufanya vurugu kwenye mechi kati yao na Burkina Faso
iliyochezwa mjini Morogoro.
Mtunza Vifaa (Kit Man) wa JKT Oljoro
FC, Eliud Mjarifu amefungiwa miezi sita na kupigwa faini ya sh. 200,000
kwa kumpiga Kocha wa Burkina Faso, CR Mwakambaya kwenye mechi kati ya
timu hizo iliyofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Pia
Mjarifu amepewa onyo kali na kutakiwa kutorudia tena kutenda kosa, kwani
hata mwenendo wake wakati wa shauri hilo ulionyesha utovu wa nidhamu
mbele ya Kamati.
Naye Mtunza Vifaa wa Rhino Rangers FC, Albert
Mbuji amefungiwa miezi sita na faini ya sh. 200,000 kwa kupatikana na
hatia ya kuwatukana na kugomea uamuzi wa marefa kwenye mechi dhidi ya
Polisi Dodoma. Adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 40(2) ya
FDL.
Kamati hiyo imeondoa malalamiko dhidi ya Ofisa Habari wa
klabu ya Ruvu Shooting, Masau Bwire kwa vile refa Israel Mujuni Nkongo
ambaye ni mlalamikaji hakufika kwenye shauri hilo.
Nkongo
alimlalamikia Bwire akidai alitoa maneno yenye kuweza kuchochea chuki
dhidi yake kwa waamuzi, kwani kupitia redio 100.5 Times FM, Bwire alidai
refa huyo ndiye aliyeshinikiza kuondolewa kwa refa Mohamed Theofil
kwenye ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).
Pia Kamati hiyo
imemkuta bila hatia Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Singida (SIREFA), Gabriel Gunda ambaye TFF ilimlalamikia kuwa akiwa
mtendaji mkuu wa chama hicho alishindwa kuhakikisha timu ya Singida
inaingia uwanjani kucheza na Dodoma kwenye mechi ya Kombe la Taifa kwa
Wanawake.
Kamati ilikubaliana na utetezi wa Gunda kuwa, jukumu la
timu hiyo lilikuwa mikononi mwa viongozi wa TWFA Singida, na tayari
SIREFA kupitia Kamati yake ya Nidhamu ilishatoa adhabu kwa viongozi wa
timu hiyo kutokana na kitendo hicho.
Nayo malalamiko ya Polisi
Tabora FC kutaka mechi yao dhidi ya Toto Africans FC irudiwe kwenye
uwanja huru (neutral ground) kwa madai ya kuchezeshwa zaidi ya muda
unaotakiwa, na kutokuwepo ulinzi wa kutosha kwenye Uwanja wa CCM Kirumba
jijini Mwanza yamekataliwa.
Pia Kamati ya Nidhamu imeelekeza
malalamiko ya timu za Mwadui FC na Polisi Mara FC dhidi ya Toto Africans
kwa kumchezesha mchezaji Ladislaus Mbogo bila kuonyesha leseni yake
yasikilizwe haraka na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kwa vile si ya
kinidhamu.
0 comments:
Post a Comment