Kocha wa klabu ya Yanga, Mdachi Hans
Van de Pluijm amesema kuwa watawashambulia wapinzani wao, BDF XI ya
Botswana mwanzo mwisho katika kipindi cha kwanza ili kupata ushindi wa
haraka katika mechi yao ya raundi ya kwanza ya kombe la shirikisho
(vilabu) barani Afrika.
Pluijm amesema wanahitaji sana ushindi wa
nyumbani ili kujiweka vizuri kwa ajili ya mechi ya marudiano
itakayofanyika baada ya wiki mbili mjini Gaborone.
Hata hivyo, kwa
mujibu wa kocha huyo, kuna uwezekano wa
nahodha wake, Nadir Haroub
“Cannavaro” kutocheza kutokana na kuumia mguu huku mshambuliaji Danny
Mrwanda akiwa na matatizo ya kifamilia.
“ Huenda watacheza kama
watapata afueni kwa matatizo yanayoyasibu, ila uwepo wao ni kwa asilimia
ndogo sana”, alisema kocha huyo.
Amesema Yanga, baada ya mechi ya
raundi ya kwanza Dar es Salaam, wataondoka Februari 27 kwenda Gaborone
kwa ajili ya mechi ya marudiano itakayochezwa siku mbili baadae ili
kupata timu itakayosonga mbele.
Maandalizi ya safari hiyo tayari
yameanza na mashabiki wa klabu hiyo kongwe, iliyotimiza miaka 80
Februari 11 mwaka huu baada ya kuanzishwa kwake mwaka 1935, wamepanga
kukodi mabasi 5 kwa ajili ya kwenda kuishabikia timu yao kwa gharama ya
shilingi 250,000 (wastani wa dola 150) kwa kila mmoja ikiwa kama nauli
ya kwenda na kurudi.
0 comments:
Post a Comment