Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewafungia kati ya mechi tatu na nane wachezaji Juma Nyoso wa Mbeya City na Aggrey Morris wa Azam kutokana na makosa ya kinidhamu waliyoyafanya wakiwa uwanjani.
Nyoso ambaye alilalamikiwa na TFF kwa kumfanyia vitendo vya
udhalilishaji mshambuliaji Elias Maguri wa Simba amefungiwa mechi nane
za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL). Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Ibara
ya 57 na Ibara ya 11 (f) ya Kanuni za Nidhamu za TFF Toleo la 2012.
Akiwa mbele ya Kamati hiyo jana (Februari 5 mwaka huu) jijini Dar es
Salaam, Nyoso alikiri kufanya
na kujutia kosa hilo, pia amemuomba radhi
mchezaji Maguri kwa kitendo hicho.
Akisoma uamuzi huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Wakili Jerome
Msemwa alisema kitendo kilichofanywa na Nyoso ni kosa kubwa,
kudhalilisha utu wa mtu, na ni mfano mbaya kwa watoto na jamii nzima ya
mpira wa miguu.
Naye Morris amefungiwa mechi tatu za VPL baada ya kutiwa hatiani kwa
kumpiga mshambuliaji Emmanuel Okwi wakati timu hizo zilipopambana kwenye
mechi ya ligi iliyochezwa Januari 25 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Kabla ya kusoma uamuzi, Wakili Msemwa alisema mlalamikiwa Morris
alikiri kugongana na Okwi, kwa maelezo kuwa aliingia kwenye ‘reli’ ndiyo
ukatokea mgongano huo.
Kamati baada ya kupitia malalamiko ya klabu ya Simba, ripoti za Brain
CT scan kutoka Besta Diagnostic Centre na nyingine kutoka Taasisi ya
Mifupa Muhimbili (MOI), taarifa za madaktari zilionyesha Okwi aligongwa
kichwani akiwa anacheza mpira na kuzimia kwa dakika tano, pia mkanda wa
video uliowasilishwa na TFF imeona kulikuwa na kugongana kati ya
wachezaji hao.
Hivyo, Kamati ikamtia hatiani Morris kwa kutumia Ibara ya 48(1)(d) ya Kanuni za Nidhamu za TFF Toleo la 2012 kwa kumfungia mechi hizo tatu na kumpa onyo kali.
Pia Kamati hiyo imemfungia miezi sita na kumpiga faini ya sh. 200,000
Meneja Vifaa (Kit Manager) wa timu ya Polisi Mara, Clement Kajeri kwa
kuhamamisha vurugu na kuwapiga waamuzi kwenye mechi dhidi ya Mwadui
iliyochezwa Uwanja wa Karume mjini Musoma. Adhabu hiyo imetolewa kwa
kuzingatia kanuni ya 40(2) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Wachezaji watatu wa Friends Rangers; Mahmoud Othman, Khalid Twahil na
John Alexander wamefungia miezi sita na faini ya sh. 500,000 kila mmoja
kwa kumpiga mwamuzi kwenye mechi ya Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya
Majimaji.
Licha ya wachezaji hao kuitikia mwito wa Kamati, wachezaji hao
walizuiwa na viongozi wa kuingia ukumbini wakati malalamiko dhidi yao
yalipoanza kusikilizwa. Hatua hiyo iliifanya Kamati ifanye uamuzi baada
ya kuusikiliza upande wa walalamikaji pekee.
Shauri dhidi ya mchezaji George Michael wa Ruvu Shooting kwa
kumchezea ubabe Amisi Tambwe wa Yanga, Kamati imeliahirisha baada ya
mlalamikiwa kupata udhuru uliosababisha asiwepo.
Pia Kamati ya Nidhamu imeelekeza malalamiko ya timu ya Friends
Rangers kupinga refa kuchezesha mechi yao dhidi ya Majimaji kwenye mvua
kubwa, kutoa maamuzi yasiyo halali na kutokuwepo na ukweli kwenye ripoti
ya Kamishna yakasikilizwe na Bodi ya Ligi kwa vile si masuala ya
kinidhamu.
0 comments:
Post a Comment