SARE tano ilizopata Simba katika mechi
zake za kwanza msimu huu zimeibua
mambo na sasa baadhi ya vigogo wa
Yanga wameweka wazi kwamba tatizo la
Wekundu hao ni mipango yao inavuja
wala si hujuma.
Mmoja wa viongozi wenye ushawishi
mkubwa ndani ya Yanga na ambaye
anajulikana kwa rekodi zake za
mapambano, ameiambia Mwanaspoti
kwamba tofauti za kimisimamo baina ya
viongozi wa juu zinachangia mambo
mengi ya ndani kuvuja na kuwapa wao
faida ndio maana mambo
yanawanyookea.
“Tunajua kila kitu kinachoendelea Simba
kwani wengine ni rafiki zetu hivyo huwa
wanatuambia nini kinafanyika katika
uongozi, kuna baadhi ya viongozi ambao
kwa sasa wamekaa pembeni na wana
urafiki mkubwa na baadhi yetu hivyo
huwa wanashirikiana mambo mengine
ikiwemo kujua siri za Simba.
“Simba haihujumiwi kama tunavyosikia,
tunapataga mipango yao mingi ya ndani
na nje ya uwanja kupitia kwa watu wao
ambao ni rafiki zetu,lakini pia tumesikia
jinsi wanavyowafukuza wachezaji wao
jambo ambalo si sahihi na wanaharibu
kabisa muelekeo wa timu, mambo ya
hujuma yapo kwa kila timu lakini
yanatakiwa kufanyiwa
uchunguzi,”alifafanua kigogo huyo
ambaye aliomba jina lake lilindwe.
Mbali na upinzani na ushabiki wa ndani
na nje ya uwanja, viongozi wa Simba na
Yanga hususani wale waliopo kwenye
kamati mbalimbali ikiwemo ya
mashindano, usajili hata za utendaji
wamekuwa na urafiki wa karibu na mara
kadhaa wameonekana kwenye vijiwe
maarufu vya Ilala na Kinondoni wakipiga
soga na kubadilishana mawazo kwenye
mambo mbalimbali.
Habari za ndani ya Simba zinadai
kwamba matokeo ya hivi karibuni
yamesababisha mgawanyiko baina ya
viongozi huku baadhi wakimshutumu Rais
wa Simba, Evans Aveva kwa misimamo
yake ya kiuongozi kwamba amekuwa
hafanyii kazi mambo anayoshauriwa na
baadhi ya vigogo wa Msimbazi.
Baadhi ya viongozi wa Simba wamezuiwa
pia kufanya mawasiliano ya moja kwa
moja na wachezaji huku wengine
wakizuiwa kukanyaga kambini na kwenye
vyumba vya kubadilishia kwa madai
kwamba wanawachanganya na kuwagawa
wachezaji jambo ambalo linaongeza
mwanya wa hujuma.
Tayari Simba imewasimamisha wachezaji
wake mahiri watatu ambao ni Amri
Kiemba, Shaaban Kisiga na Haroun
Chanongo kwa maelezo kwamba
wanawachunguza kwa sababu mbalimbali
na wakishajiridhisha watawarudisha
ingawa uwezekano wa wachezaji hao
kuvaa tena jezi ya Simba mwaka huu ni
finyu.
Mbali na Simba kudai kwamba kuna watu
wanatumika kuhujumu ndani kwa ndani,
sababu nyingine ambayo wamekuwa
wakiieleza ni kwamba baadhi ya
wachezaji wao wameanza kuchuja.
Simba itacheza mechi ya sita kesho
Jumamosi dhidi ya Mtibwa Sugar, mechi
itakayofanyika Uwanja wa Jamhuri
mkoani Morogoro ambapo viongozi wa
Simba wametoa tahadhari kwa wachezaji
wao kwamba endapo matokeo yakiwa
mabaya basi wachezaji wengine
wanaotuhumiwa watafungashiwa virago
vyao huku benchi la ufundi likipewa
mechi mbili kuanzia wikiendi hii
kujirekebisha.
0 comments:
Post a Comment