Kamati ya Waamuzi nchini imemuondoa refa
msaidizi namba moja, Ferdinand Chacha
kuchezesha mechi ya watani wa jadi, Yanga
na Simba, na nafasi yake sasa inachukuliwa
na Samuel Mpenzu kutoka Arusha ambaye
atasaidiana na John Kanyenye kwenye
mchezo huo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania
Bara ambao mwamuzi wa kati atakuwa Israel
Nkongo.
Hata hivyo, mabadiliko hayo yaliyofanywa na
kamati hiyo yalichelewa kufika katika
sekretarieti ya Shirikisho la Soka nchini (TFF),
ambayo juzi ilimtangaza Chacha na Kanyenye
wa Mbeya kuwa watamsaidia Nkongo katika
mechi hiyo namba 27 itakayopigwa Uwanja
wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini
jana kutoka kwa chanzo chetu muhimu ndani
ya kamati hiyo, zinaeleza maamuzi ya
kumuondoa mwamuzi huyo yametokana na
'shinikizo' kutoka kwa viongozi wa klabu ya
Yanga ya jijini ambao wanadaiwa kumkataa
Chacha ambaye pia aliwachezesha katika
mechi yao ya kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar
iliyofanyika mkoani Morogoro.
Taarifa zaidi zinadai kwamba Yanga
iliwasilisha maombi ya kumkataa Chacha kwa
kamati na hatimaye mwamuzi huyo mwenye
beji inayotambuliwa na Shirikisho la Soka
duniani (Fifa) kuondolewa.
Habari zaidi kutoka kwa chanzo chetu
ziliendelea kueleza kwamba baada ya Yanga
kumkataa, mwamuzi huyo alitakiwa kuandika
barua ya kuomba aondolewe kuchezesha
mechi hiyo lakini Chacha hakuwa tayari
kufanya hivyo.
Hata hivyo, kiongozi mmoja wa juu wa TFF
anadaiwa naye kushiriki katika mabadiliko
hayo ya kumuengua Chacha kwa kumueleza
kwamba asilazimishe kuuchezesha mchezo
huo wa watani wa jadi kwa sababu unaweza
kuharibu rekodi yake.
Mwenyekiti wa Kamati wa Waamuzi nchini,
Salum Chama, aliliambia gazeti hili kwa njia
ya simu kuwa ni kweli kamati hiyo imefanya
mabadiliko lakini hayatokani na shinikizo
lolote.
Chama alisema sababu kubwa ni kubaini kuwa
Chacha alichezesha mechi kati ya Mtibwa
Sugar na Yanga ambayo ilimalizika kwa kikosi
cha Mbrazil Marcio Maximo, kuchapwa mabao
2-0.
"Kamati ndiyo yenye maamuzi ya kupanga na
kubadilisha mwamuzi, tumepangua kwa
sababu tumeona si vyema mwamuzi mmoja
kuambatana na timu moja ndani ya muda
mfupi, hakuna sababu nyingine kama
ulivyoniuliza," alisema Chama kwa kifupi.
Lakini kwa upande wa Mkurugenzi wa
Mashindano wa TFF, Boniface Wambura,
alisema shirikisho halihusiki na mabadiliko
hayo.
Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto,
hakuwa tayari kuelezea madai hayo.
Rais wa Simba, Evance Aveva, alisema "yote
sawa, kama wameamua kumbadilisha sisi
kwetu mpira ni dakika 90".
0 comments:
Post a Comment