728x90 AdSpace

  • Latest News

    Monday, October 06, 2014

    KEN ASTON MGUNDUZI WA KADI ZA NJANO,NYEKUNDU MICHEZONI

    Habari na Paul Manjale
    Kennedy George ``Ken" Aston hili si jina maarufu sana midomoni na masikioni mwa mashabiki wa mpira wa miguu duniani hasa katika ukanda huu tuliopo lakini katika vitabu vya FIFA jina hili liko ukurasa wa mbele kabisa pengine kuliko hata jina la raisi wa sasa wa shirikisho hilo Sepp Blatter.


    Moja kati ya sababu ya kutofahamika kwa mtu huyu katika kizazi hiki nadhani ni kwakuwa bado dunia inatafuta jibu sahihi la nani mkali kati ya Messi na Ronaldo baada ya kuumaliza kiurahisi ule mjadala wa nani jembe kati ya Pele mwenye medali tatu za kombe la dunia dhidi ya Maradona mwenye medali moja ya michuano hiyo shingoni mwake.

    Je ken ni nani hata niache shughuli zangu nyingine na nianze kumzungumzia yeye jumapili hii ya leo?

    Ken Aston alizaliwa 1 Septemba,1915 huko Englandalikuwa ni mwalimu,mwanajeshi,jaji na  mwamuzi aliyekuja na wazo la matumizi ya kadi za njano na nyekundu kwenye mchezo wa soka.

    Aston  akisimulia jinsi  alivyopata wazo hilo anasema


    `Ilikuwa ni katika  mchezo wa robo fainali wa kombe la dunia la mwaka1966 kati
    ya Argentina na  England nilimuona mwamuzi mwenzangu Rudolf Keirtlin (Mwamuzi toka Ujerumani) akipata wakati mgumu kumtoa nje ya uwanja mshambuliaji na nahodha wa Argentina Antonio Rattin aliyekuwa amemfanyia madhambi mchezaji mmoja wa England"

    Rudolf hakuwa akijua kiagrentina hivyohivyo Rattin nae hakujua kijerumani basi ikawa ni kituko pale uwanjani kifupi hakukuwa na maelewano ikanibidi nitoke pale nilipokuwa nimekaa na kuingia uwanjani kumshawishi Rattin atoke ili mchezo uendelee.

    Baada ya mchezo huo uliopigwa Wembley kumalizika tulikaa kupitia mambo kadhaa likiwemo tukio la Rattin kugomea kutolewa uwanjani huku pia ripoti ya mwamuzi Rudolf ikionyesha kuwa wachezaji wa England ambao ni ndugu Bobby na Jack Charlton nao walikuwa ni wakosefu (Offenders) katika mchezo ule lakini adhabu yao haikuwa kuwatoa nje.Kilichokuja kunichosha zaidi ni Rudolf kusema kingine kilichochangia yeye kumtoa nje Rattin ni kwamba alihisi mchezaji huyo alimtuka wakati wakizozana,ikumbukwe Rudolf alikuwa hajui hata neno moja la kispania.(Argentina wanatumia kispania kama lugha yao ya taifa)


    Kutokana na mkanganyiko huo nilianza kurudi nyumbani Lancaster nikiwa na mawazo tele ghafla nikasimama baada ya taa za kuongozea magali katika makutano ya Kensington high street kuwaka taa nyekundu ikiwa ni ishara kutaka tusimame.Wakati nikisubiri taa hizo zituruhusu tuendelee na safari nikaanza kuzikodolea macho taa hizo jinsi zinavyofanya kazi mpaka tuliporuhusiwa kuondoka.

    Nilipofika nyumbani nilimuelezea mke wangu Hulda kila kitu kilichojiri jioni ile na fikra zangu juu ya zile taa za barabarani lakini kabla sijamaliza kumsimulia yote Hulda aliondoka na kwenda kwenye chumba kimoja tulichokuwa tukikitumia kama stoo na baada ya dakika chache alirudi akiwa na vipande viwili vya karatasi ngumu za kujengea.Vipande hivyo kimoja chekundu na kingine cha njano vilikuwa vimekatwa katika ukubwa ambao ilikuwa rahisi kuviweka na kuvitoa mfukoni.Nikaviweka mfukoni mwangu vile vipande na kuanza kuvitoa kimoja baada ya kingine nikifuatisha  taa za barabarani kwamba njano jiandae na nyekundu ondoka.
    Nikawafuata wenzangu na kuwaambia juu ya hilo wazo langu la  kuwa na ishara ambayo itakuwa wazi kwa wote ili kuondoa usumbufu kama alioupata bwana Rudolf pale Wembley.

    Baada ya wazo hilo kukubalika tulizitumia kadi hizo kwa majaribio katika michuano ya soka ya Olympiki ya mwaka 1968.Miaka miwil baadae yaani mwaka 1970 ndipo yalipoanza matumiz ya kadi hizo kwa Mara ya kwanza katika kombe la dunia lililofanyika huko Mexico huku mwaka 1982 zikaanza pia kutumika rasmi katika ligi zote duniani.

    Je,ugunduzi wa Aston uliishia kwenye kadi pekee?

    Hapana,Aston akionyesha kweli yeye ni mtu wa mabadiliko na maboresho mwaka 1966 baada ya kadi pia alikuja na wazo la kuwepo kwa mwamuzi wa akiba kama tahadhari ikiwa yeyote kati ya wale waamuzi  watatu atapata tatizo litakalomfanya ashindwe kuendelea na mchezo.


    1974,Aston alikuja na wazo la kutumia ubao wenye namba wakati wa kufanya mabadiliko ya wachezaji (substitution) badala ya kuitana majina kwamba flani toka flani aingie.Nikikurudisha nyuma mwaka 1947,Aston alitambulisha matumizi ya vibendera vyekundu na njano kwa waamuzi wa pembeni (linesman) kwa madai kuwa rangi hizo zinaonekana vizuri hata mtu akiwa mbali.

    Kwanini Marekani inamuabudu?

    Huwezi kuzungumzia soka la Marekani bila kumtaja Ken Aston kwani toka mwaka 1980-2001 alikuwa na kazi moja tu nchini humo ambayo siyo nyingine bali kuendesha mafunzo ya uwamuzi pamoja na kuzitafsiri sheria 17 za mchezo wa soka ambaye yeye alikuwa ni miongoni mwa  waandaaji wa sheria hizo.

    Je,unaukumbuka mchezo ulioweka rekodi ya kuwa na kadi nyingi zaidi nyekundu na njano?

    Mchezo huu ulipachikwa jina la utani la Battle of Nuremberg.Huu ulikuwa ni mchezo wa mtoano wa kombe la dunia )la mwaka 2006 huko Nuremberg,Ujerumani kati ya Ureno na Uholanzi ambapo mwamuzi Valentin Ivanov alitoa jumla ya kadi 16 za njano na kadi nyekundu 4 katika mchezo huo uliojaa ubabe wa kila namna.Wareno walishinda goli 1-0.Baada ya mchezo huo kuisha akiwa na hasira raisi wa FIFA Sepp Blatter alimtuhumu mwamuzi huyo kuwa aliuharibu mchezo huo kwa kutoa kadi hovyo na kusema hata mwamuzi huyo na yeye alistahili kujipa kadi.Baadae Blatter alimwomba radhi mwamuzi huyo
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: KEN ASTON MGUNDUZI WA KADI ZA NJANO,NYEKUNDU MICHEZONI Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top