MFUNGAJI Bora wa Ligi Kuu Bara msimu
uliopita, Amissi Tambwe, kwa sasa
anaonekana si lolote katika timu yake ya
Simba ambapo amefunga bao moja tangu
msimu huu uanze, lakini imebainika
kuwa mfumo anaotumia kocha wao
Patrick Phiri ndio chanzo cha
kuporomoka kwa straika huyo.
Mchezaji huyo ambaye ameanza
kuwatamanisha baadhi ya viongozi wa
usajili wa Yanga, ametamka kwamba
anamalizia mechi zake mbili zilizobaki
Simba kufunga mwaka halafu arudi kwao
Burundi ambako anaweza kufanya
uamuzi mgumu kutokana na vitisho
alivyopata klabuni kwake hivi karibuni.
Habari za ndani zinadai Tambwe ambaye
amebakiza miezi mitano katika mkataba
wake ameanza kujadiliwa na baadhi ya
vigogo wa Yanga ambayo tayari ina
wachezaji watano wa kigeni, lakini
mtihani ni jinsi ya kumshawishi kocha
Mbrazili Marcio Maximo.
Hata hivyo mabosi hao wanadai watajua
cha kufanya baada ya kumaliza mechi
zilizosalia mwaka huu na kusikia
tathmini ya Kocha.
Wakati Simba
ilipokuwa chini ya kocha, Zdravko
Logarusic, kocha huyo alikuwa hampi
majukumu mengi Tambwe huku kazi yake
kubwa ikiwa ni kukaa eneo moja na
kusubiri mipira ya kufunga ambapo
alikuwa kitumia mifumo ya straika
mmoja mbele 4-5-1 au 4-2-3-1.
Lakini Phiri amempa Tambwe majukumu
mawili ambapo anashuka kutafuta mipira
na kupanda kufunga jambo ambalo
limekuwa gumu kwake kumudu
majukumu mawili kwa wakati mmoja.
Phiri hupendelea sana kutumia mifumo
ya 4-4-2, 4-3-3 na 3-5-2.
Tambwe alikiri kuwa mabadiliko hayo pia
yamechangia kiwango chake kuonekana
kushuka kwani hawezi kufanya yote hayo
kwa wakati mmoja. “Kila kocha ana
mfumo wake wa ufundishaji, nilipokuwa
chini ya Loga sikuwa na majukumu
mengi katika timu, lakini hivi ninapewa
majukumu mengi ambayo si rahisi
kuyafanya kwa wakati mmoja na kuleta
mafanikio, hivyo nalazimika kucheza
kutokana na kocha anavyotaka,” alisema
Tambwe.
Tambwe pia ni miongoni mwa wachezaji
wanaotuhumiwa kucheza chini ya
kiwango kutokana na matokeo ya sare
tano mfululizo huku akitajwa kuwa ni
mmoja wa wachezaji watakaotemwa kwa
kosa hilo ambapo yeye amesema kwamba
yupo tayari kuondoka ili kupisha wengine
watakaoisaidia Simba.
“Nipo katika wakati mgumu sana kwa
sasa, tuhuma zimezidi jambo ambalo si
kweli, nakosa amani ndani ya timu hivyo
sioni sababu ya kuendelea kuwepo sehemu
ambayo maisha yangu yapo hatarini,
maisha ya mpira ndivyo yalivyo lakini
kwa sasa yamezidi maana imefikia hatua
natumiwa ujumbe wa vitisho, sasa
nasubiri nini Simba? Nataka nikapumzike
kidogo,” alisema Tambwe
Tambwe pia alikuwa mfungaji bora katika
michuano ya Kombe la Kagame alipokuwa
na timu yake ya Vital’O ya Burundi 2013
yaliyofanyika Sudani Kusini ambapo
alifunga mabao sita.
Lakini Phiri, alisema hupenda kutumia
mifumo hiyo ili timu iweze kushambulia
zaidi na kupata mabao, pia alikiri
wachezaji wengi wameathirika
kisaikolojia kutokana na matokeo
wanayoyapata.
0 comments:
Post a Comment