KOCHA wa zamani wa Makipa wa Simba,
Idd Pazi, amesema sasa ni muda mwafaka
kwa kipa, Juma Kaseja, kurejea kwenye
kikosi cha klabu yake hiyo ya zamani
kutokana na uzoefu mkubwa alionao.
Hivi karibuni kumekuwapo na taarifa za
Kaseja kurejeshwa kwenye kikosi cha
Simba ili akasaidiane na kipa chipukizi,
Peter Manyika Jr pamoja na Hussein
Shariff ‘Casillas’ kwani Ivo Mapunda
anahusishwa na mpango wa kutemwa
kikosini hapo.
Pazi ambaye hivi karibuni aliondolewa
kuinoa Simba baada ya klabu hiyo
kushindwa kupata matokeo mazuri
kwenye mechi za Ligi Kuu Bara, alisema
Kaseja anaweza kuisaidia klabu hiyo
lakini ameutaka uongozi wa kutatua
matatizo mengine yanayochangia klabu
hiyo kufanya vibaya.
“Kaseja ni kipa mzoefu, ataisaidia Simba
hivyo siyo jambo baya kumrejesha, pia
amekuwa na historia nzuri na klabu hiyo
kwa muda wa miaka 10 aliyokuwa pale,”
alisema.
“Hii pia itamsaidia Manyika ambaye
ndiyo kwanza anakua, kuna mechi
ambazo anaweza kudaka lakini nyingine
ni lazima adake kipa mwenye uzoefu.”
Akizungumzia matokeo mabaya
yanayoikabili Simba kwa sasa, Pazi
alisema viongozi wanafahamu kiini cha
tatizo, lakini wamegoma kuyatafutia
ufumbuzi jambo linaloendelea
kuigharimu timu.
“Kuna mambo ya nje ya uwanja ambayo
yanachangia timu kuboronga, viongozi
wanayafahamu lakini ni kama
wameyafumbia macho, wajitahidi
kuyatafutia ufumbuzi ndipo wawaze
kufanya usajili,” alisema Pazi.
0 comments:
Post a Comment