728x90 AdSpace

  • Latest News

    Wednesday, December 31, 2014

    IVAN WA SANTIAGO,ZAMORANO WA CHILE

    Ukifika leo katika jiji la Santiago nchini Chile jiji linalosifika kwa kuwa na sura nzuri ambayo ni kishawishi tosha kwa mgeni yoyote yule kutamani asirudi mapema alikotoka  ukataja jina ``Ivan El Terrible" ama ``Bamm Bamm" hata mtoto mdogo aliyeko chekechea leo hii atajua tu yakwamba una muongelea mfalme wa mji huo,mfalme wa soka la Chile Ivan Luis Zamorano Zamora.Mkongwe mwenye miaka 47 sasa aliyerudi Santiago kupumzika baada ya kuchafua hali ya hewa ya soka la Ulaya na jezi yake namba 1+8.
    Nyota anayeshikilia nafasi ya 249 katika orodha ya nyota 250 bora wa muda wote kuwahi kutokea.Licha ya kucheza soka wakati ule soka likiwa halilipi vizuri sana kama ilivyo leo Zamorano anabaki kuwa mfalme  tena juu ya wafalme wa Chile wanaotamba kwa sasa duniani kama Alexis (Erdilla de Tocopilla) na Athuro Vidal (Il Guerriero) kwa mambo mengi sana.


    Machache kati ya hayo mengi ni kuwa amewatangulia wafalme hao kucheza soka Ulaya.Wakati Zamorano akitua Uswisi kukipiga na klabu ya St Gallen,Sanchez alikuwa kwao Pacopilla.Alikuwa mdogo sana hata kiganjani hajai,Vidal yeye alikuwa kwao San Joaquín akiwa mduchu kama kirikuu tena wakati huo akiwa bado anafuta kamasi kwa shati.Zamorano hakuwahi kunyoa kiduku wala panki kama ilivyo kwa vijana hao niliowataja hapo juu El terrible alibaki na nywele zake zilizomwagika kama mkia wa farasi.
    Kubwa zaidi inasemekana Zamorano ndiye mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea nchini Chile huku pia shingoni mwake akiwa na medali ya michuano mikubwa ya Ulaya.

    Aondoka Chile atinga Ulaya kusaka mahela.

    Mwaka 1988 Zamorano alitua Uswisi kukipiga klabu ya Fc St Gallen akitokea klabu ya nyumbani kwao ya Cobresal na kufunga jumla ya magoli 34 katika michezo 56.

    1991 Atua Hispania kukipiga na Sevilla.

    Baada ya kufanya vizuri na klabu ya Fc St Gallen klabu ya Sevilla ilimnunua Ivan Zamorano na kufanikiwa kuifungia magoli
    21 katika  michezo 59 kabla ya kutua Real Madrid kwa kitita cha dola milioni 5.

    Real Madrid
    Akiwa na Real Madrid mwaka 1992 -1996,Zamorano alitwaa taji moja la La Liga,taji moja la Copa del
    Rey,na taji moja la Spanish Supercup.Mwaka
    1995, chini ya kocha Jorge Valdano ,
    Zamorano aliisaidia Real Madrid kutwaa taji la La Liga, akifunga magoli 27 ikiwemo hat–trick dhidi ya FC Barcelona na kufanikiwa kutwaa tuzo ya Pichichi tuzo ambayo hutolewa kwa mfungaji bora wa La Liga. Katika msimu wa 1992–93 na 1994–95 Zamorano alitwaa tuzo ya EFE.Tuzo ambayo hutolewa kwa mchezaji bora asiye raia wa Hispania.Jumla Zamorano aliichezea
    Real Madrid, michezo 137 na kuifungia magoli 77.



    Atua Inter Milan baada ya misimu mitano kutesa La Liga.

    Zamorano atua Italia apewa jezi namba 9 na kukipiga kwa misimu minne katika ligi ya Serie A na Internazionale,toka mwaka 1996 mpaka 2000 na kucheza na wakali kama Youri
    Djorkaeff, Diego Simeone , Javier Zanetti,
    na Ronaldo.Wakati huo bila kucheza Italia bado haujaonekana kama mchezaji uliyekamilika.

    Afanya kituko baada ya kupokonywa jezi namba 9.

    Baada ya kuivaa muda mfupi klabu ya Inter ilimsajili mshambuliaji hatari wakati huo Roberto Baggio ambaye  moja kati ya ushawishi wa kutua Giussepe Meazza ilikuwa ni pamoja na kupewa jezi namba 10 aliyokuwa akiihusu kuliko kitu chochote.



    Kichwa kikawauma mabosi wa inter ambao hawakutaka kumkosa Baggio wala kumkwaza Ronaldo De Lima ambaye kwa wakati huo dunia ilikuwa miguuni mwake huku akipewa jeuri na kampuni ya Nike.Bahati mbaya ikimwangukia Zamorano ambaye ilibidi aivue jezi namba 9 ampe Ronaldo kisha naye aitoe jezi namba 10 kwa Roberto Baggio.

    Baada ya Inter kumnyang'anya Zamorano jezi yake namba  9 na kumpa namba 18.Zamorano aliongeza alama ya + kati ya 1 na 8 na jezi yake kusomeka 1+8 ambayo kimahesabu ilibaki kuwa namba 9.Mei 1998,aibebesha Inter taji la
    UEFA Cup baada ya kuifungia goli moja kati ya ushindi wa magoli 3-0 dhidi ya Lazio.

    Jina Ivan El Terrible lilitoka wapi?
    Kutokana na umwamba wake katika kufumania nyavu za wapinzani Zamorano alipewa jina la utani lililokuwa likitumiwa na mtawala wa zamani wa Urusi wa miaka ya 1530-1584 Ivan IV Vasilyevich.



    Huyu ndiye Ivan Zamorano anayejinoa kiualimu na kikosi cha vijana cha Chile (U-18) kabla ya kuitia mikononi timu ya taifa ya wakubwa hapo siku za usoni.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: IVAN WA SANTIAGO,ZAMORANO WA CHILE Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top