STRAIKA aliyechukua hatamu kwenye
fowadi ya Simba, Mganda Emmanuel
Okwi, amesisitiza kwamba hana tofauti na
mchezaji yeyote wa Simba na anatamani
kucheza pamoja na mshambuliaji
anayeanzia benchi, Mrundi Amissi
Tambwe.
Thamani ya Tambwe ambaye alikuwa
straika namba moja wa Simba msimu
uliopita, imeshuka kutokana na mfumo
wa kocha Mzambia Patrick Phiri ambao
umemfanya aanzie benchi ingawa katika
mchezo wa Jumapili dhidi ya Ruvu
Shooting kwenye Uwanja wa Taifa ana
nafasi kubwa ya kuanza.
Tambwe ambaye alikuwa mfungaji bora
msimu uliopita, sasa anaanzia benchi na
Phiri anapenda kumtumia zaidi Okwi kwa
maelezo kwamba ana kasi, nguvu na
anajua kutumbukiza mipira nyavuni
tofauti na staili ya Tambwe ambaye ni
mviziaji na akikutana na mabeki wabishi
timu hukwama.
Ingawa uongozi umekanusha kwa nguvu,
lakini kumekuwa na maneno kwamba
thamani ya Tambwe ndani ya Simba
imeshuka baada ya Okwi kutua na
kwamba mchezaji huyo anafikiria kuingia
mitini kwenye dirisha dogo la usajili
litakaloanza Novemba 15 licha ya
kwamba uongozi unajitahidi kumuweka
fiti kisaikolojia.
Okwi aliyetua Simba akitokea Yanga
aliyositisha nayo mkataba, alisema hana
tatizo katika kucheza na Tambwe katika
kikosi cha kwanza na Phiri amekiri
kwamba atawapanga.
Okwi alisema anapocheza na Tambwe
katika kikosi kimoja safu ya ushambuliaji
yao inakuwa na makali zaidi. “Sina tatizo
katika kucheza na Tambwe pale mbele
wala mchezaji mwingine yeyote,
nakumbuka kuna mechi tuliyocheza
pamoja mimi na Tambwe tulielewana
sana nikajikuta nimebanwa na mabeki
lakini Tambwe akawa sehemu safi
nikampa krosi akafunga kirahisi
kabisa,”alisema Okwi ambaye amekuwa
akijituma sana katika mechi za
hivikaribuni mpaka kufikia hatua ya
kucheza na majeraha.
Kwa upande wake Phiri alisema: “Kuna
mechi nakumbuka walicheza pamoja
Tambwe akafunga, lakini hapa kati
sikuwa nawapanga pamoja kuna mambo
nilikwa najaribu kuyapanga sasa Okwi
anaumwa lakini akipona tutaangalia
uwezekano wa kuweza kuwatumia tena
kucheza pamoja katika mechi ijayo.”
Katika mazoezi ya juzi Jumatano ya kikosi
hicho, Phiri alionekana kumjaribu
Tambwe katika kikosi ambacho kinaweza
kuanza Jumapili huku Okwi akianza
mazoezi taratibu peke yake ambapo
uwezekano wa kuwepo mechi ijayo
itategemea na maendeleo ya maumivu
yake.
0 comments:
Post a Comment